November 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rushwa yasababisha chaguzi 3 CCM kusimamishwa

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo

Spread the love

 

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesimamisha chaguzi tatu kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali ikiwemo za rushwa zilizoibuliwa, ili kuchukua hatua kwa ajili ya kutenda haki kwa wagombea na wapiga kura. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yameelezwa leo Jumatatu, tarehe 21 Novemba 2022 na Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, akizungumza na wanahabari jijini Dodoma, kuhusu uchaguzi wa ndani wa chama hicho ngazi ya mkoa.

Chongolo ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Uchaguzi CCM, ametaja uchaguzi wa kwanza ulisomamishwa ili kupisha uchunguzi, ni wa nafasi ya mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Mkoa wa Mbeya, wa pili ni wa mjumbe wa NEC Arusha.

“Tumesimamisha uchaguzi wa nafasi ya mjumbe wa NEC Mkoa wa Mbeya, kwa sababu ya tuhuma mbalimbali zikiwemo za Rushwa na yenyewe tunafanya uchunguzi wa kina. Tukikamilisha tutafanya uamuzi wa chama. Tumesimamisha uchaguzi wa mjumbe wa NEC Arusha, nayo tatizo ni hilo,” amesema Chongolo.

Uchaguzi wa tatu ambao umesimamishwa kwa tuhuma za rushwa ni wa Mkoa wa Kichama wa CCM, Magharibi Zanzibar, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za mwanachama mmoja kuchukua box la kura na kulipeleka katika chumba cha kuhesabia kura.

“Pia, kuna uchaguzi uliofanyika jana mkoa wa kichama wa Magharibi Zanzibar, ambapo kumekuwa na malalamiko ya baadhi ya wagombea na wajumbe wakieleza kuhusiana na tukio la moja ya wanachama kuchukua box la kura kwenda nalo kwenye chumba kilichokuwa kimeandaliwa kwa ajili ya kuhesabia kura,” amesema Chongolo.

Chongolo amesema “kuna malalamiko tunataka kujua uchukuaji wa box hilo ulikuwa unalenga kwa ajili ya kuhesabia kura au kulikuwa na lengo lingine. Tutafuatilia tukijiridhisha tutachukua uamuzi. Tukijiridhisha kulikuwepo na lengo lingine tukijiridhisha tutachukua uamuzi tutafuta uchaguzi na kurudia upta.”

Katibu Mkuu huyo wa CCM amesema, uchunguzi huo ukikamlika taarifa yake itapelekwa katika vikao vya chama kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.

“CCM kinafanya maamuzi kwa vikao na yale yanayohusisha makala ya kikatiba kama hayo niliyokuwa nayo mkurugenzi, nachukua hatua kwa kufuata taratibu tulizojiwekea wenyewe ndiyo maana sijasema nimefuta uchaguzi, nimesema nimesimamisha ili uchunguzi ukamilike na kuvishauri vikao kuchukua hatua,” amesema Chongolo.

Chongolo amesema, changamoto iliyopo katika chaguzi hizo, ni baadhi ya wanachama aliowaita wajanja wakiwemo wagombea na wapambe wao, kutengeza msukumo wa kuonyesha wanaungwa mkono na viongozi wa chama hicho. Amesema hakuna mgombea wa kiongozi kwani wote wameteuliwa na CCM.

Amesema, ili kukabiliana na changamoto hizo, CCM kimepeleka viongozi na maafisa wake katika kila mkoa, kwa ajili ya kufuatilia kwa karibu chaguzi hizo na kudhibiti vitendo vya udanganyifu.

“Chama kimetuma maafisa na viongozi kuwa wasimamizi wa uchaguzi kila mkoa kwenye mikoa yote nchini. Hatujaacha mchakato kuendelea bila sisi kuwepo. Kwa hiyo kuna jicho letu kila mkoa lakini pia mikoa tuliyosimamisha chaguzi zinaendelea kwa ngazi nyingine ambazo hatujachukulia hatua,” amesema Chongolo.

error: Content is protected !!