August 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rushwa ya ngono yatibua

Spread the love

KUKUA na kushamiri kwa rushwa ya ngono nchini kumeendelea kupigiwa kelele na watu mbambali nchini, anaandika Charles William.

Miongoni mwao ni Mtandao wa Jinsia hapa nchini (TGNP) ambao umeeleza kukerwa na kushamiri kwa vitendo hivyo.

Kutokana na kushamiri kwake, TGNP imewaomba Watanzania wote bila kujali jinsia zao kukabiliana na vitendo hivyo.

Kwa kutambua ukweli kuwa tatizo la rushwa ya ngono linazidi kuwa kubwa, TGNP imeendesha kongamano la kujadili suala hilo hii leo jijini Dar es Salaam kwa kutoa mbinu mbalimbali namna bora ya kukabiliana na vitendo hivyo.

Katika kongamano hilo pia wanawake kutoka maeneo mbalimbali walitoa ushuhuda juu ya namna walivyokabiliana na changamoto ya kuombwa au kulazimishwa rushwa ya ngono wakiwa katika ofisi zao za kazi.

Akizungumza na wanahabari mara baada ya kongamano hilo kumalizika, Grace Kisetu, Kaimu Mkurugenzi wa TGNP amesema kuwa, kongamano hilo limelenga kuwapa ujasiri wanawake na wanaume juu ya namna ya kukabiliana na rushwa ya ngono kuanzia nyumbani, shuleni na hata katika ofisi zao za kazi.

“Suala la rushwa ya ngono kwa sasa sio la wanawake tu, hata wanaume wapo wanaoombwa rushwa ya ngono na wanawake katika baadhi ya maeneo ili waweze kufanikishiwa mambo yao, kwa hiyo tunatoa elimu kwa wote ili kwa pamoja tuweze kuvidhibiti vitendo hivi vinavyoshika kasi,” ameeleza Kisetu.

Dk. Ave Maria Semakafu ambaye alikuwa mmoja kati ya watoa mada katika kongamano hilo, amesema suala la rushwa ya ngono ni moja kati ya mambo ambayo yapo kila mahali kwa sasa lakini yanaonewa aibu kuzungumzwa na kukemewa kwa uwazi na hivyo kufanya lizidi kukua kwa kasi.

“Tumebaini kuwa rushwa ya ngono kwa sasa ipo kuanzia mahakamani, mashuleni, maofisini, kwenye vyama vya siasa na hata katika majumba zetu tunaona wasichana wa kazi wa ndani wakiombwa rushwa ya ngono na watoto wa kiume wa mwajiri wake au baba mwenye nyumba hii ni hatari sana”. Ameeleza Dk. Ave na kuongeza;

“Imefika mahali wanafunzi wa sekondari wanamwita mwalimu wao wa kiume ‘shemeji’ kwa kuwa, wanajua anatembea na mwanafunzi mwenzao ambaye huvujishiwa mitihani na yeye anawapatia wenzake kwahiyo kila mahali sasa ni rushwa ya ngono”.

Hata hivyo Dk. Ave hakueleza ni matukio mangapi ya rushwa ya ngono ambayo TGNP imeweza kuyabaini au kuripotiwa na kueleza kuwa kikwazo kikubwa ni wanawake pamoja na wanaume kutokuwa tayari kuyafikisha masuala husika katika vyombo vya kisheria kwa kuogopa aibu na fedheha.

Kongamano hilo lililofanyika makao makuu ya TGNP lilikuwa na kauli mbiu ya “Vunja Ukimya, rushwa ya ngono inadhalilisha na inaua” huku likihudhuriwa na watu wa makundi mbalimbali wakiwemo wanafunzi, wazazi na wanaharakati wa masuala ya usawa wa kijinsia.

error: Content is protected !!