WANAFUNZI wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati wametahadharishwa, kwamba wasipokuwa makini rushwa ya ngono itawaharibia maisha yao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Iringa…(endelea).
Kauli hiyo imetolewa na Mweli Kilimali, Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Iringa akizungumza na klabu za wapinga rushwa za vyuo vikuu na vya kati mkoani humo.
Ametoa kauli hiyo kutokana na kuwepo kwa taarifa za kukithiri kwa rushwa ya ngono vyuoni, na kwamba wametakiwa kutowafumbia macho walimu na wahadhiri wanaojihusisha na tabia hiyo.
“Nawataka wanafunzi kuacha tabia ya uvivu wa kujisomea ili mfanye vizuri katika mitihani yenu, mkifanya hivyo mtaepuka kuwashawishi wahadhiri katika rushwa ya ngono au fedha, lakini sio wote wanatoa rushwa ya ngono,” amesema.
Amesema, ubaya wa rushwa ulianzia katika vitabu vya dini ambapo Qur’an Tukufu na Biblia Takatifu, zote zimekema vitendo hivyo vya rushwa vyenye maudhui ya kupora haki.
“Ndugu zangu, rushwa ni adui, rusha ni mbaya, rushwa imekemewa katika vitabu vyetu vitukufu ndani ya Qur’an Tukufu na katika Biblia Takatifu. Rushwa hii ya ngono inavunja utu na kumdhalilisha mtenda na mtendewa, hivyo kataeni rushwa,” amesema.
Profesa Gaudence, Mkuu wa Kitivo cha Elimu katika Chuo Kikuu cha RUCU, alikiri kuwepo kwa vitendo hivyo vyuoni na kuwataka wanafunzi kuacha woga, badala yake watoe taarifa kwa vyombo vinavyoshughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia katika ngazi za chuo, polisi au Takukuru.
Martha Magembe, Mshauri wa Wanafunzi wa RUCU amewataka wanafunzi hao kutokuwa chanzo cha rushwa ya ngono, kwa kutoa ushawishi kwa wahadhiri wao.
“Kuna baadhi ya wanafunzi wanafanyiwa vitendo vya kikatili lakini wananyamaza kutokana na woga, au kuhofia kupoteza kitu fulani kutokana na vitisho hivyo, nawaomba mtoe taarifa Takukuru ili tuwabaini wahusika na sheria ichukue mkondo wake,” amesema.
Leave a comment