December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rushwa CCM: Donda lililokosa dawa

Jakaya Kikwete

Jakaya Kikwete, Mwenyekiti wa CCM aliyemaliza muda wake

Spread the love

RAIS Jakaya Kikwete amekiri chama chake kushindwa mapambando dhidi ya rushwa. Amesema, “Kama hatutabadilika katika suala la rushwa, mwaka 2015 tutakuwa na wakati mgumu sana.”

Amenukuliwa akikiri kuwa iwapo mwaka huo “tutafanikiwa kuishika serikali, basi mwaka 2020 katu hatutarudi tena madarakani.”

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo Ijumaa iliyopita, mjini Dodoma. Alikuwa akifunga mafunzo maalumu ya siku nne kwa makatibu wa mikoa, makatibu na wenyeviti wa wilaya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka kote nchini.

Amesema, “Najua rushwa ipo na mnaendelea kupokea shilingi laki mbili za airtime (muda wa mawasiliano). Ndugu zangu hatutafika; ama wengine watavuka na wengine kukwama.”

Amekabidhi kazi ya kushughulikia wala rushwa ndani ya chama chake kwa Philip Mangula, makamu mwenyekiti wa CCM, Tanzania Bara.

Hii ni mara ya kwanza rais kukiri hadharani kwamba rushwa itakiondoa chama chake madarakani. Kwa miaka mingi, Rais Kikwete amekuwa akilaani waliokuwa wanatabiri kifo cha CCM kwa sababu ya kukumbatia rushwa. Aliwahi kusema wanaotabiria chama chake kufa kwa rushwa, watatangulia wenyewe.

Kwa mpangilio wa sasa, mwenyekiti wa CCM, chama ambacho kinatawala, ndiye mkuu wa vyombo vya dola. Anachozungumza anakifahamu kwa kuwa amesheheni taarifa nyingi na nyeti kuhusu mwenendo wa chama chake na nchi.

Hata hivyo, madai dhidi ya wanaowania madaraka kutumia fedha kununua uongozi, hayakuanza kutolewa leo.

Kwa miaka mingi, wanachama na baadhi ya viongozi wamekuwa wakiwashutumu baadhi ya wanaotafuta madaraka – kuanzia yale ya kiserikali hadi ya kichama – kununua uongozi kwa kutumia fedha. Madai haya hayakushughulikiwa.

Katika kinyang’anyiro cha kutafuta mgombea urais wa chama hicho mwaka 2005, baadhi ya wanachama walishutumiwa kutumia fedha kusaka uongozi. Miongoni mwa waliodaiwa kutumia fedha kusaka madaraka, ni Jakaya Mrisho Kikwete.

Aliyedaiwa kumwaga fedha kwa niaba ya mgombea Kikwete, ni Rostam Aziz, mbunge wa zamani wa Igunga, mwekahazina mstaafu wa CCM na mmoja wa wamiliki wa makampuni ya Dowans Holding Limited, Dowans Tanzania Limited na Richmond Development Company (DRC).

Alikuwa kada wa chama hicho, Joseph Butiku, aliyeeleza kinagaubaga hatari ya matumizi ya fedha kwenye uchaguzi. Katika andishi lake kwa aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Benjamin Mkapa, Butiku alituhumu viongozi wake kunyamazia rushwa na kupindisha kanuni za uchaguzi.

Alisema ukimywa ni sawa na “kubariki vitendo hivyo.” Katika kile kilichokuja kuitwa baadaye “Waraka wa Butiku kwa Mkapa,” mkurugenzi huyo wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere alisema, Mkapa na wenzake, akiwamo Mangula, wamekizamisha chama hicho mahali ambako hakiwezi tena kurejea mstalini.

Hakuna aliyemsikiliza Butiku. Aliishia kushambuliwa na kutukanwa. Wengine walimwita mnafiki na kusema, “Andishi lake limetokana na hasira ya kushindwa kwa mgombea wake.” Inadaiwa chaguo lake wakati huo alikuwa Dk. Salim Ahmed Salim. 

Naye Mangula aliwahi kulalamika mwaka 2007, jinsi fedha za rushwa zilivyomuondoa kwenye kinyang’anyiro cha uenyekiti mkoa wa Iringa. Alisema katika uchaguzi huo, hakuna anayeweza kusimama na kusema – kuanzia kiongozi wa kitaifa hadi mjumbe wa shina – “kuwa nimeshinda bila rushwa.” 

Akiongea kwa sauti ya uchungu, Mangula alisema, “Wakati wa kampeni, nilitengeneza vipeperushi kurahisisha kazi ya kuwafikia wajumbe. Lakini wapigakura waliniambia, ‘hatutaki vipeperushi vyako. Tunataka vipeperushwa.’” Alisema, hapo ndipo chama chake kilipofikia.

Baada ya uchaguzi kumalizika, Mangula alidai ule haukuwa uchaguzi. Ulikuwa ni ulanguzi wa kura. Akakiomba chama chake kufanyia kazi madai yake na mengine yanayohusu uchaguzi na ununuzi wa uongozi. Hakuna kilichotendeka.

Madai ya rushwa yameibuka mara nyingi ndani ya mikutano ya NEC. Kwa mfano, kuna wakati baadhi ya viongozi wa chama hicho, akiwamo aliyekuwa mtendaji mkuu, Yusuph Makamba walituhumiwa kuvuruga uchaguzi kwa maslahi binafsi.

Makamba alijibu madai hayo kwa kusema, “Kila mgombea wa ubunge na udiwani ametoa rushwa, isipokuwa walizidiana viwango.”

Waziri mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye amelalamikia rushwa. Aliwahi kusema kuwa kile kinachoitwa na viongozi wake, “Uchaguzi mkuu wa ndani ya chama,” hakikuwa uchaguzi. Alikiita ununuzi wa kura.

Sumaye alikuwa akizungumzia kilichotokea kwenye uchaguzi wa mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya taifa, wilaya ya Hanang. Sumaye alishindwa kwa kile kilichoitwa, “nguvu ya fedha.”

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, baadhi ya wagombea walitumia jina la ikulu na rais na kudai kuwa wamejitosa katika kinyang’anyiro kwa kuwa walitumwa na Rais Kikwete.

Hata hivyo, wananchi walipowagundua waliwakataa. Miongoni mwa waliopitishwa lakini wananchi wakagoma kuwachagua, ni Ramadhani Madabida ambaye aligombea ubunge katika jimbo la Kilwa Kusini.

Alishindwa katika kura za maoni. NEC ilirejesha jina lake. Hatimaye jimbo la Kilwa Kusini likaangukia kwa Chama cha Wananchi (CUF).

Kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge jimboni Arumeru Mashariki, madai ya rushwa yaliibuka kwenye hatua ya kura ya maoni. Kamati Kuu (CC) ya CCM ilisikiliza tuhuma hizo zilizowakabili baadhi ya wagombea.

Taarifa zinasema, ushahidi thabiti uliwasilishwa mbele ya kikao. Mjumbe mmoja wa CC alitajwa kusaidia kugawa rushwa. Lakini mwenyekiti Kikwete hakukubaliana na waliopendekeza kubatilishwa kwa matokeo.

Aliagiza wagombea wawili walioongoza kura za maoni, kurudishwa kwa wanachama kupigiwa kura kwa mara ya pili ili apatikane mshindi. Ni baada ya uchaguzi wa awali, kukosekana mgombea aliyefikia nusu ya kura zilizopigwa.

Uchaguzi mkuu wa Umoja wa Vijana (UV-CCM), nao uligubikwa na madai ya rushwa. Paul Makonda aliyegombea nafasi hiyo, alimtuhumu mwenyekiti wake, Sadifa Hamisi Juma, kutumia fedha kushinda uenyekiti. Hakuna hatua zilizochukuliwa.

Baadaye Makonda ameibuka kwenye nafasi ya Katibu Uhamisishaji wa UVCCM taifa. Aliyemtuhumu kushinda uongozi kwa ununuzi wa kura, ndiye amemteua yeye kushika nafasi hiyo. Kuna wanaosema malalamiko yamezaa cheo.

Kwenye uchaguzi wa wabunge wa Afrika Mashariki, taifa lilishuhudia viroja vya wabunge kuhongana. Rais kama vile alimnukuu Makamba, alijibu kwa ufupi, “Hatuna la kufanya kwa sababu wote wametoa rushwa, ila wamezidiana viwango.”

Kauli ya rais ni uthibitisho kwamba anajua na kukubali wawakilishi waliotumwa katika bunge la Afrika Mashariki, wengi wao ni watoa rushwa wakubwa.

Kwa dola makini, ingetosha kufuta uchaguzi ule na kuitisha uchaguzi upya kwa misingi mipya. Kama angefanya hivyo, angerejesha kidogo heshima ya chama chake iliyotota. Hata katika hili la kutaka kuondoa wagombea wanaonunua uongozi, angepata mahali pa kuanzia. 

Katika uchaguzi mkuu uliopita ndani ya CCM, madai ya ununuzi wa kura yaliwakumba hata wale waliotangazwa washindi bila kupingwa. Wengi wao walidaiwa kutisha wagombea wengine; kuwanunua waliotaka kujitokeza kuwapinga na kutumia jina la rais.

Waliopita bila kupingwa ni pamoja na Ridhiwani Kikwete na Salma Kikwete. Wakati Ridhiwani alitangazwa kushinda bila kupigiwa kura wilayani Bagamoyo, naye Salma alitangazwa kushinda mkoani Lindi.

Hakika, kelele za rushwa zipo kila mahali. Bali wapo wanaolalamika kwa dhati; wapo wanaosema kwa kebehi na wapo wanaofanya usanii.

Hii ni kwa sababu, historia ya hongo kwenye uchaguzi wa chama hiki, ilianza kwa kugawa khanga, fulana na kofia aina ya kapero. Sasa wanatoa rushwa fedha taslimu katika mamilioni ya shilingi. Wengine wanagawa hadi fedha za kigeni kwa lengo la kuvutia wapigakura.

Hata Edward Lowassa, waziri mkuu aliyejiuzulu kwa kashifa ya Richmond, ambaye ndiye anadaiwa kuwa mlengwa wa hotuba ya Kikwete; naye analalamikia rushwa kwenye chama chake.

Katika moja ya taarifa zake kwa vyombo vya habari kupinga rushwa, Lowassa anasema:

“Nikiwa mwana-CCM na Mtanzania, ninasononeshwa sana na taarifa za kukithiri kwa vitendo vya rushwa ndani ya chama chetu, serikalini na katika taasisi mbalimbali.

“Ni kweli kwamba rushwa ni tatizo. Ni kansa ambayo kama taifa, hatuna budi kuitafutia ufumbuzi wa kimfumo badala ya kuendelea kufikiri kwamba inaweza kumalizwa kwa njia ya kulalamika, kulaumiana na kupakana matope.

“Tunao wajibu wa kuhakikisha kwamba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), inapewa meno na kuimarishwa zaidi katika kukabiliana na vitendo hivi vya ukiukwaji wa maadili.”

Katika mazingira haya, nani anaweza kumfunga paka kengele? Yupi anaweza kunyooshea kidole mwenzake? Kila mmoja analalamika. Mlalamikiwa yuko wap?

Lowassa huyu anayelalamikia rushwa, ndiye anayedaiwa kutafuta uongozi kwa udi na uvumba. Ndiye huyuhuyu aliyekuwa mwenyekiti wa kundi la wanamtandao liliomuingiza Kikwete madarakani mwaka 2005.Mtandao wa Kikwete ulitumia njia hiyohiyo ambayo sasa wanaitumia kutaka kumuweka Lowassa madarakani.

Lakini kuna hili pia. Mangula anamfahamu vizuri mwenyekiti wake. Anajua nguvu waliyonayo wanaonunua uongozi. Anajua jinsi alivyopoteza wadhifa wake wa ukatibu mkuu wa chama mara baada ya Mkapa kung’atuka uongozini mwaka 2006.

Anajua na bila shaka, bado anakumbuka, jinsi Mkapa alivyozuia ripoti ya kamati ya maadili; alivyolazimisha maamuzi ya chama kufanywa nje ya vikao; alivyobadilisha kanuni za uchaguzi kutoka mjumbe mmoja kura tatu, hadi mjumbe mmoja kura moja.

Anajua utaratibu huo mpya uliletwa na Mkapa ndani ya mkutano. Haumo kwenye kanuni za chama; haukuwahi kujadiliwa na vikao vya chama; wala kuelezwa kwa wajumbe kabla ya mkutano wa  uchaguzi.

Lakini kusema ni jambo moja. Kuaminika ni jambo jingine. Rais Kikwete ameshindwa kuchukua hatua ya kuwafukuza kutoka kwenye chama au hata kuwapa barua za onyo, baadhi ya watuhumiwa ufisadi.

Kutochukua hatua kumefuatia maapizo ya viongozi wenzao kuwa “lazima mafisadi watoswe.” Je, mtu huyo anawezaje kusimamia kazi itakayofanywa na Mangula; iwapo Mangula atakuwa ametembelewa na ujasiri, aghalabu kwa muda tu?

Kuna wanaosema anaweza kuiachia njiani. Si ajabu ukasikia mwenyekiti amemwachia makamo wake kuendesha kikao ili kukimbia kulaumiwa.

Katika mazingira hayo, kazi yoyote itakayofanyika sasa kwa lengo la kuokoa chama, haiwezi kukisaidia kuvuka hapa kilipo. Uamuazi wowote wa kujivua gamba kwa njia hii, una uwezekano wa kuondoka hadi ngozi yenyewe. Tusubiri tuone.

error: Content is protected !!