June 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rufaa za kina Mdee hatihati kusikilizwa Chadema

Halima Mdee

Spread the love

 

HATIMA ya kufanyika au kutofanyika kwa kikoa cha Baraza Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), utajulikana kesho Jumamosi, tarehe 24 Julai 2021. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kikao hicho, kilichokuwa kimetangazwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kufanyika tarehe 31 Julai 2021, jijini Mbeya, kiko hatihati kufanyika baada ya Mbowe kukamatwa na polisi.

Mbowe na wenzake 11, walikamatwa saa 8 usiku wa kumamia tarehe 21 Julai 2021, katika Hotel ya Kingdom jijini Mwanza, walipofikia kwa ajili ya kuhudhuria kongamano la kudai katiba mpya.

Mara baada ya kukamatwa, walipelekwa kituo kikuu cha polisi Mwanza huku Mbowe akisafirishwa kwenda Dar es Salaam kwa mahojiano ambapo Polisi wamedai anatuhumiwa kupanga njama za mauaji ya viongozi na ugaidi.

Leo Ijumaa, tarehe 23 Julai 2021, Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, Tundu Lissu akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao ‘Zoom’ amewema, hatima ya baraza hilo itajulikana kesho.

“Kuhusiana na baraza kuu, tulipanga kufanya tarehe 31 Julai 2021 na masuala yote yanyofanywa na baraza yangefanyika. Kamati kuu imepanga kufanya kikao chake kesho na baada ya kesho sasa tutatoa uamuzi.”

“Kwa hiyo itakutana kuzungumzia hatma ya baraza kuu, sasa mwenyekiti wetu amekamatwa yumo ndani hatujui hatma yake. Haya maamuzi tutayafanya katika kikao ambacho kimeitishwa kwenye kikao mahsusi, majibu yatapoatikana kesho,” Lissu.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, Tundu Lissu

Amesema hayo, akijibu swali aliloulizwa na MwanaHALISI Online, lililotaka kujua maandalizi ya baraza hilo yanaendelea ikiwemo kuwajulisha waliokuwa wanachama wao Halima Mdee na wenzake 18, kufika kusikiliza rufaa zao.

Miongoni mwa mambo yaliyopangwa kujadiliwa katika mkutano wa baraza hilo, ni rufaa ya Halima Mdee na wenzake 18, waliowasilisha Chadema, kupinga kutimuliwa ndani ya chama hicho.

Walifukuzwa tarehe 27 Novemba 2020 na kikao cha kamati kuu, kilichokutana kuwajadili kwa tuhuma za usaliti, kughushi nyaraka za chama na kujipeleka bungeni kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum.

Mbali na Mdee, wengine waliofukuzwa Chadema, ni waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Ester Bulaya na Esther Matiko; aliyekuwa Katibu Mkuu Bawacha, Grace Tendega; aliyekuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Vijana (Bavicha), Nusrat Hanje na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Baraza hilo (Bara), Hawa Mwaifunga.

Katika orodha hiyo, wamo pia aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Bawacha (Bara), Jesca Kishoa; aliyekuwa Katibu Mwenezi wa Bawacha, Agnesta Lambat; aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mtwara, Tunza Malapo na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Bawacha, Zanzibar, Asia Mohamed.

Wengine ni Cecilia Pareso, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Salome Makamba, Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza, Felister Njau na Stella Siyao.

error: Content is protected !!