August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rufaa ya serikali ndoa za utotoni yashangaza

Spread the love

WANAMTANDAO wa mashirika yanayopinga ndoa za utotoni, wameshtushwa na rufaa iliyotolewa na serikali ya kupinga uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania kesi iliyohusu ndoa za utotoni, anaandika Regina Mkonde.

Mwanzoni mwa mwaka huu, Rebeca Gyumi, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Msichana Initiative, alifungua shauri katika Mahakama Kuu ya Tanzania kuhoji uhalali wa baadhi ya vifungu vinavyoruhusu ndoa za utotoni.

Katika hukumu iliyotolewa tarehe 8 Julai 2016 iliitaka serikali kufanya marekebisho na kufuta vifungu husika.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Valerie Msoka, Mwenyekiti wa TECMN amesema kuwa, mtandao huo unashindwa kuelewa dhumuni la rufaa hiyo kutokana na kwamba, walitegemea kuona kuwa serikali inatekeleza agizo la mahakama kwa lengo la kutokomeza ndoa za utotoni.

“Tunajiuliza maswali mengi na kushindwa kuelewa rufaa hii inabebwa na misingi gani, na je kweli serikali yetu inataka kuendelea na vifungu vya kisheria vinavyoruhusu watoto wa kike kuolewa chini ya umri wa 18?” amehoji Msoka na kuongeza;

“Tumekusanyika hapa leo kuonesha kushtushwa, kushangazwa na kusikitika kwetu baada ya kuona taarifa iliyotolewa na mwanasheria mkuu wa serikali ya kukata rufaa katika mahakama ya rufani ili kupinga maamuzi yaliyotolewa na mahakama kuu kwenye kesi hiyo.

“Ikumbukwe kuwa, mwanzoni mwa mwaka huu Taasisi ya Msichana Initiative ambayo ni mwanachama wa mtandao huu ilifungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu ya Tanzania.”

Amesema katika kesi hiyo mlalamikaji alikuwa anahoji uhalali wa kikatiba wa vifungu namba 13 na 17 vya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 vinavyoruhusu mtoto wa kike kuolewa akiwa na miaka 14 au 15 kwa ridhaa ya wazazi au ya mahakama.

“Kama watetezi wa haki za haki za watoto na wanaopinga ndoa za utotoni hapa nchini, tulifurahishwa na hukumu ya shauri hilo iliyotolewa mapema julai 8, 2016 chini ya jaji kiongozi Shaban Lila.

“Lila  alisema kuwa, vifungu hivyo kweli siyo halali na ni kinyume cha katiba na kuitaka serikali kufanya marekebisho na kufuta vifungu hivyo ndani ya mwaka mmoja.”

Msoka amesema wanamtandao huo wanaikumbusha serikali kuwa ina wajibu wa kulinda raia na kulinda haki za makundi mbalimbali katika jamii na kwamba ili hayo yaweze kufanikiwa ni lazima iwepo misingi imara ya kisheria na ya kiutawala ili kuhakikisha sheria zinasimamiwa.

error: Content is protected !!