May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

RPC Tanga ataja chanzo ajali DC Korogwe

Spread the love

KAIMU Kamanda Polisi Mkoa wa Tanga, David Mwasimbo amesema chanzo cha ajali ya gari aliyopata Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Basila Mwanukuzi jana mkoani Tanga, ni uzembe wa dereva wake. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Akizungumza na MwanaHalisi Online leo tarehe 8 Mei, 2022 Kamanda Mwasimbo amesema ajali hiyo ya gari imetokea jana tarehe 7 Mei, 2022 katika barabara ya Tanga-Segera eneo la Hale wilayani humo.

 

Amesema dereva wa Mkuu huyo wa wilaya alishindwa kulimudu gari hilo aina ya Toyota Land cruiser kutokana na mwendokasi alipokuwa akijaribu kuyapita magari mengine hali iliyosababisha kupata ajali.

Amesema ndani ya gari hiyo mbali na dereva pamoja na Mkuu huyo wa wilaya pia alikuwapo kijana mmoja ambaye ni msaidizi wa Ofisi ya Basila.

Amesema dereva na kijana huyo wamepata majeraha madogo lakini Mkuu wa wilaya hiyo ya Korogwe kwa upande wake aliumia vidole vya mguu wa kushoto na shingo baada ya mkanda wa usalama ndani ya gari kumkaba.

Aidha, amesema hali za majeruhi wote zinaendelea vizuti na hadi sasa wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Tanga, Bombo.

Aidha, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Bombo, Dk. Jonathan Gudemo amekiri kuwapokea majeruhi watatu wa ajali hiyo akiwemo mkuu huyo wa wilaya.
Dk.Gudemo amesema majeruhi wawili hali zao zinaendelea kuimarika akiwemo Mkuu wa Wilaya na bado wapo chini ya uangalizi wa matabibu.
“Majeruhi mmoja tumempatia rufaa ya kwenda Muhimbili (Hospitali ya Taifa Muhimbili) kwa ajili ya matibabu zaidi,amesema Dk.Gudemo.
error: Content is protected !!