July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

RPC, RC Dodoma wawatisha wapigakura

Spread the love

JESHI la Polisi mkoa wa Dodoma na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Ghallawa wamewatishia wananchi kuwa watawadhibiti wakati wa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Hali hiyo imejitokea kutokana na jeshi hilo kutangaza kikosi cha ukakamavu pamoja na kuwadhibiti wapigakura watakaofanya fujo huku mkuu wa mkoa akidai kuna timu ya ukaguzi kwa wapigakura.

Hayo yanaonekana kuwa mpango mkakati wa kuwatishia wapigakura kutokana na jeshi hilo kutoa mafunzo ya ukakamavu kwa askari wake ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.

Mafunzo hayo ni kwa ajili ya maandalizi ya kujihami na vurugu ambazo zinazoweza kutokea kutokana na mihemko ya wafuasi wa vyama mbalimbali vya siasa mkoani hapa.

Hayo yalielezwa jana na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Dodoma, David Misime katika mkutano wa viongozi wa dini jana ambao uliitishwa na Ghallawa.

Misime amesema licha ya askari kujifunza mafunzo ya ukakamavu pia wamejifunza sheria na haki za binadamu na haki za mpigakura.

“Tumejiandaa kuwalinda wanaopigakura kwa amani na kuwakabili wale wanaojiingiza kwenye vurugu,” amesema.

Amesema polisi watatumia nguvu ile ile itakayofanywa na watu watakaosababisha vurugu katika zoezi hilo.

“Tutaenda na nguvu hiyo hiyo unayotumia, ukirusha mawe na si tunarusha mawe na sio ya kuokota,” alijigamba Misime.

Wakizungumza kwenye mkutano huo, viongozi wa dini waliitaka serikali kutenda haki kwenye uchaguzi mkuu ili kuepuka uvunjifu wa amani.

Pamoja na Misime kujitamba kuwa jeshi limefundishwa ukakamavu na kuhakikisha linatumia nguvu nyingi kupambana na wananchi bado viongozi wa dini walionekana kupingana na hali hiyo.

Katika kuhakikisha kwamba viongozi wa dini hawaungi mkono, Askofu wa makanisa ya Pentekosti, Donald Kahango amesema wasimamizi wa uchaguzi na watendaji wahakikishe wanatenda haki katika uchaguzi kwani bila kutendeka kwa haki kuna uwezekano mkubwa amani ikapotea.

Naye Shekhe Shaban Kitlya wa Msikiti wa Nungwi mjini hapa, alieleza kwamba vitabu vitakatifu vinaeleza kuwa moja ya sababu ya uvunjifu wa amani ni dhuruma na unyang’anyi na kuwataka kuhakikisha hayo hayajitokezi.

Akijibu hoja hizo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Gallawa, aliwahakikishia viongozi hao serikali itasimamaia haki kabla, wakati wa zoezi la kupiga kura, kuhesabu na kutangaza matokeo ya uchaguzi.

“Taarifa nilizozipata kuna watu kutoka nje ya Dodoma wanakuja kwa ajili ya kufanya fujo kwenye uchaguzi tutawadhjibiti na tumeunda timu ya kukagua,”amesema.

Aidha, Gallawa alisema katika vituo vya kupiga kura kutakuwa na mistari mitatu ya wanawake, wanaume na watu wenye mahitaji maalum.

error: Content is protected !!