August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

RPC Msangi atamba Mwanza

ACP Ahmed Msangi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza

Spread the love

AHMED Msangi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza (RPC) ametamba kwamba, vitendo vya uhalifu wa kutumia silaha za moto vinavyofanya na watu wachache vitakomeshwa, anaandika Moses Mseti.

Amesema, hali ya usalama kwa sasa mkoani humo ipo vizuri na kwamba, Jeshi la Polisi limejipanga kuiendeleza.

Katika kipindi cha miezi miwili, Mwanza imekuwa na matukio mbalimbali yanayotishia amani wakazi wake.

Katika kipindi hicho watu zaidi ya 11 wameuawa kwenye matukio tafauti ikiwemo kuchinjwa kinyama na watu wasiofahamika.

Kauli hiyo imetolewa leo na Kamanda Msangi wakati wa ufunguzi wa kampeni ya kuhamasisha vyombo vya habari nchini kupiga vita uhalifu, ilioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari wa kupiga vita dawa za kulevya na uhalifu Tanzania (Ojadact).

Kamanda Msangi ambaye pia ni Kamishna Msaidizi wa Polisi (SACP) amesema kuwa, hivi karibuni kumekuwepo na matukio mbalimbali ya uhalifu wa kutumia silaha, kitendo ambacho kinaonesha kuwapa wasiwasi wananchi.

Amesema kuwa, pamoja na polisi kuweka mipango na mikakati ya kudhibiti vikundi vya wahalifu mkoani humo, aliwaomba wanahabari kuendelea kushirikiana na polisi katika kuibua watu wanaojihusisha na uhalifu ili kujenga mkoa wenye amani na utulivu.

“Unajuwa mkoa wowote ule ambao una amani na utulivu, hata shughuli za kimaendeleo zitakuwepo, tunapaswa kuwa pamoja katika kuimalisha usalama wa Mkoa wa Mwanza na lengo la serikali ya awamu ya tano ni kufikia uchumi wa katika ifikapo mwaka 2025.

“Kama mkoa hauna amani hata uchumi wetu utakuwa duni na hakuna mtu atakaekuja kuwekeza katika mkoa huu ninawaomba wanahabari ushirikiano wenu na kama kuna mwekezaji anataka kuja kuwekeza Mwanza aje amani ipo,” amesema Msangi.

Edwin Soko, Mwenyekiti wa Ojadact amesema, wameamua kuzindua kampeni hiyo kwa wanahabari ili wao waweze kutoa elimu kwa wananchi namna ya kulipoti matukio ya uhalifu katika maeneo yao.

Amesema endapo wananchi watakuwa na elimu juu ya kulipoti matukio ya uhalifu, vitendo hivyo vitapungua katika mkoa huo kama sio kuisha kabisa huku akiwasisitizia wanahabari hao kutoa elimu kwa Wananchi na kuandika habari zinazojenga jamii.

 

error: Content is protected !!