September 23, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Royal tour’ ya Rais Samia yaanza kumiminia watalii, KITS wachangamkia fursa

Afisa Uendeshaji Mkuu wa Kampuni ya kimataifa inayojihusisha na masuala ya utalii ya Kilimanjaro International Tourism & Safaris (KITS), Francis Malugu

Spread the love

 

WAKATI filamu ya ‘Royal Tour’ ikiwa katika maandalizi kabambe kutangaza vivutio vya utalii Tanzania, Kampuni ya kimataifa inayojihusisha na masuala ya utalii ya Kilimanjaro International Tourism & Safaris (KITS), inatarajia kupokea ugeni wa mawakala wa utalii zaidi ya 30 kutoka nchi za Marekani, Ufaransa na Lithuania kuanzia Novemba 23, 2021. Anaripoti Patricia Kighono, TUDARCo … (endelea).

Kampuni hiyo ya KITS pia ni balozi na lango la kuingiza watalii na wawekezaji kutoka majimbo 50 ya Marekani.

Akizungumzia na waandishi wa habari leo tarehe 13 Septemba 2021 jijini Dar es salaam, Afisa Uendeshaji Mkuu wa Kampuni ya KITS, Francis Malugu amesema mawakala hao wa utalii watawakilisha maelfu ya watalii kutoka nchi hizo kuja Tanzania.

Amesema ujio wa mawakala hao umechangiwa kwa kiasi kikubwa na hatua ilizochukua KITS baada ya kuona taarifa za Rais Samia Suluhu Hassan akishiriki kutengeneza makala ya filamu ya kutangaza vivutio vya utalii duniani ijulikanayo kama “Royal Tour” ambayo kwa awamu hii imefanyika nchini Tanzania.

Mkurugenzi wa Wellworth Hotel, Sameer Ismail,

Amesema kazi ya kuwataarifu Mawakala hao wa utalii kuhusu filamu hiyo ya ‘Royal Tour’ ilifanywa na kampuni hiyo ya KITS, yenye Makao Makuu yake jijini Washington, DC nchini Marekani na ofisi zake za uendeshaji zilizo jijini Arusha.

“Baada ya kupata taarifa za utengenezaji wa filamu huku Rais Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kuwa muongozaji mkuu, tuliwataarifu mawakala wa Utalii katika vyama vya utalii duniani ambavyo KITS ni mwanachama wake na zaidi ya mawakala 30 walithibitisha kuja kuitembelea Tanzania, Novemba mwaka huu,” anasema Malugu.

Pia alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Samia kwa uamuzi aliouita wa busara na wa makusudi wa kuitangaza Tanzania kupitia ziara hiyo maarufu ya “Royal Tour.”

Kaimu Mkurugenzi wa Masoko Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Felix John

Akielezea sababu za kupongeza uamuzi huo wa Rais, Malugu amesema kwamba utasaidia kuongeza nguvu katika utekelezaji wa azma ya Serikali ya kukuza uwekezaji na kuvutia utalii kama ambavyo KITS imekuwa ikifanya nchini Marekani.

“Kukamilika kwa makala ya filamu hiyo itasaidia kurahisisha shughuli za utangazaji utalii  ambazo kampuni ya KITS imekuwa ikizifanya katika nchi mbalimbali,” amesema.

Aidha, ametaja mikutano na matukio ya kimataifa watakayoshiriki kuwa ni pamoja na Oktoba 10 hadi 11 mwaka huu nchini Ufaransa katika onesho la ‘Top Resa’, Travel Adventure Show itakayofanyika majiji ya Atlanta, Georgia na San Francisco, California.

“Tukio jingine kubwa tunalokwenda kushiriki ni pamoja na National Tour Association (NTA) Annual Convention linalofanyika jijini Clevelend, Ohio ambalo litahusisha mawakala wa utalii zaidi ya 2,300 kutoka majimbo yote ya Marekani na nchini Canada.

“Ni matarajio yetu kuwa kama makala hiyo itakuwa imekamilika katikati mwa Novemba, KITS itatumia ushawishi wake kueneza kwa wateja wake juu ya kuonyeshwa kwa makala hiyo ya Rais Samia wakati wa tukio la ufunguzi wa Kongamano hilo.” amesema.

Mkurugenzi wa Wellworth Hotel, Sameer Ismail,

Aidha, kwa niaba ya Mwenyekiti na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya KITS, Vonnie Kiondo, Francis Malugu ametoa shukrani za dhati kwa ushirikiano ambao kampuni yao imekuwa ikipewa na mamlaka mbalimbali za serikali ukiwemo ubalozi wa Tanzania nchini Marekani.

Pia Bodi ya Utalii Tanzania, Mamlaka za Hifadhi za TANAPA, TAWA na Ngorongoro, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Kituo cha Mikutano cha kimataifa cha Arusha (AICC) taasisi ambazo zina dhamana ya kuendeleza utalii na wadau wakubwa katika shughuli za kuvutia uwekezaji na utalii nchini.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa Masoko kutoka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB),  Felix John ameishukuru Kampuni hiyo KITS kwa kuchangamkia fursa zinazoendelea kujitokeza katika sekta ya utalii.

Amesema hatua hiyo inazidi kuipa morali serikali katika kuhakikisha inafikia lengo la kufikia watalii milioni tano ifikapo mwaka 2025 na kukusanya mapato ya zaidi ya dola za Marekani bilioni sita.

error: Content is protected !!