August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Roma: Hatupo salama, aeleza mateso waliyopata

Roma Mkatoliki (katikati) akizungumza na waandishi wa habari

Spread the love

MSANII wa muziki wa Hip-Hop Ibrahim Mussa ‘Roma Mkatoliki’ aliyetekwa na watu wasiojulikana kisha kuachiwa akiwa na wenzie watatu amesema hawapo salama kwa kilichowakumba, anaandika Hamisi Mguta.

Roma amesema hayo leo katika mkutano wake na wanahabari kuelezea kilichotokea katika tukio zima la kutekwa kwao na kuwa baada ya kutekwa na watu hao, walifungwa vitambaa usoni na kupelekwa sehemu ambayo hata wao hawakuitambua.

“Hali hii muda wowote inaweza ikarudi, lakini pia iwe fundisho kwa watu wengine kwa sababu muda wowote inaweza kutokea kwa yoyote, kama imetokea kwa daktari, ikaja ikatokea kwa msanii usishangae kesho ikamkuta mwandishi wa habari au kiongozi wa siasa,” amesema.

Msanii huyo akiwa ameambatana na Mkewe, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Harrison Mwakyembe pamoja na wenzake aliotekwa nao, amegoma kutaja maswali waliyoulizwa na watekaji hao ambayo yaliambatana na kipigo kama alivyoeleza.

“Tukio limetokea kweli na tumeumia, tumepigwa ndiyo maana tunasema hali yetu ya ulinzi Dar es Salaam haiko vizuri, lakini kwa bahati nzuri ni kwamba tukio lote tumesharipoti kwenye vyombo vya Dola kuanzia siku ya jumamosi wameanza kufanya upelelezi, sheria zetu ni kwamba upelelezi unapoanza huruhusiwi kusema chochote,” amesema.

Amesema kuwa kilichotokea kinasababisha mwenzao Binladen anapata tabu ya kushituka usiku kwa kukumbuka tukio lililowatokea na anatisha wengine.

Akizungumza huku akitetemeka hali inayoonesha kuwa hayuko sawa, amesema kuwa siku zote tatu walizokaa sehemu wasiyoifahamu walikuwa wanafanyiwa mahojiano ambayo yaliambatana na vipigo.

Hata hivyo amesema kuwa habari zinazoendelea kusambaa zinawasikitisha kutokana na kuwa hazina uhalisia wa kilichowakuta.

“Kuna watu waamini hakuna kilichotokea, wanasema tumetengeneza kiki kwa maslahi binafsi na wengine wanaenda mbali kusema tunatumika kisiasa huku wengine wanaongea kama wanajua kilichotokea, amesema Roma na kuongeza:

“Tumeumia sana kuna baadhi ya wasanii na watu wanasema kuwa tumepewa hela kufanya hivyo, sisi ni masikini sana hatuwezi kuhatarisha maisha yetu kwa sababu ya pesa, siko sawa kiafya na hata wenzangu, unaona mwili wangu (akionesha majeraha yaliyotokana na vipigo).

“Si kitu cha mchezo na inauma kusikia mtu anasema tumepewa dola elfu 5 kufanya hayo mambo, hofu yangu ni kwamba narudije kwa jamii, kama wameshaanza kunipa shutma hizo, mama wazazi wangu hali ni mbaya sana kwa sababu wanaamini mtoto wao hayupo salama.”

Wameeleza kuwa baada ya kuteswa walitelekezwa sehemu maeneo ya Ununio sehemu ambayo waligundua baada ya kutembea umbali wa kiasi kutoka walipotupwa, wakiwa wamefungwa macho, baadaye kuwasiliana na Mkurugenzi wa Clouds Media Group Luge Mutahaba ambaye ndiye aliwasaidia kuwafikisha Oysterbay Polisi.

Waziri Mwakyembe amesema atashangaa kama chombo cha dola kikigundulika kuhusika na kuwakamata wasanii hao bila ya kuelezwa yeye kama mlezi wa wasanii.

“Wenzetu wameomba upelelezi tuwape msaada, nimwaombe ushirikiano wenu wote tumestushwa na hii sio hali ya kawaida nchini kwetu na hii si kwa wasanii wa muziki tu, hawa ni bendera ya Tanzania, wawakilishi wa Tanzania,” amesema Mwakyembe.

Ingawa Mwakyembe alionekana kusita kujibu swali la mmoja wa mwandishi aliyeuliza kuwa ‘ikibainika ni kweli vyombo vya ulinzi vimefanya kazi ya kuwakamata utafanyaje? Mwakyembe alikwepa kujibu swali hilo na kusema kuwa anaulizwa maswali ya kina Bashe (Hussein, Mbunge wa Nzega Mjini).

kuhusu Makonda alichokisema kuwa kina Roma alipoulizwa kuhusu kauli ya uongozi wa mkoa ya kusema kuwa wasanii hao wataonekana kabla ya Jumapili analichukuliaje swala hilo, Mwakyembe akawa mgumu haki kutaka asikilizishwe kilichoongelewa na uongozi mkuu wa mkoa.

Amesema “wasanii wetu wanahaki ya kujieleza kama sheria ya nchi inavyoeleza, pamoja na kwamba inaweka masharti ya kutokuvuka mipaka, wasanii mkipata tatizo lolote ambalo hakijakaa kiserikali serikali niulizeni niwataarifu na Basata tupate majibu ya haraka,” amesema.

Hadi sasa bado hawajafahamikia ni kina nani waliwateka wasanii hao huku likiendelea kuleta ugumu wa kutambuliwa kwao baada ya wasanii kutowataja wahusika waliomkamata na wenyewe kushindwa kuwatajaa wala kusema sababu waliyotekewa kwa kigezo cha kusubiri uchunguzi.

 

error: Content is protected !!