WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), umewahimiza wananchi kutumia mfumo wa kielektroniki wa utoaji vyeti, badala ya kuwatumia vishoka ambao wanasababisha wapate vyeti vya kughushi ‘feki’. Anariopoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Meneja Masoko na Mawasiliano wa RITA, Josephat Kimario, akizungumza na MwanaHALISI Online, ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Kimario amesema, mfumo huo unaofahamika kwa jina la E-Huduma, ulioanza kutumika 2019, unasaidia wananchi kupata huduma za RITA, popote walipo.
“Tumeboresha huduma zetu kwa lengo la kuhakikisha zinawafikia watu wengi hasa wa vijijini, ambao kwa muda mrefu wamepata changamoto ya kupata huduma zetu. Ambapo mfumo wa zamani ilikuwa lazima mwananchi aende kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya kufanya maombi na kupata cheti,” amesema Kimario.
Aidha, Kimario ametoa wito kwa wananchi kusajili matukio muhimu kama ya vizazi, vifo na ndoa, ili kuondoa usumbufu utakaojitokeza kutokana na kukosa cheti za tukio husika.
“Tusajili kwa wakati matukio, badala ya kusubiri vikihitajika tunaanza kukurupuka na kutafuta vyeti ili tutimize mahitaji yetu,” amesema Kimario.
Wakati huo huo, Kimario amewaomba wananchi waepuke kutumia njia za panya katika kutafuta vyeti, ili kutokomeza tatizo la uwepo wa vyeti feki.
“Unakuta cheti kilitafutwa na mzazi siku za nyuma, wazazi walitumia njia za mkato. Mtu anakuja anakwambia nipe hela nitakusaidia kupata cheti, mzazi anakaa nacho anaridhika kuwa mtoto ana cheti, kikija kuhakikiwa unakuta feki,” amesema Kimario na kuongeza:
“Tunawasihi wazazi wasitumie njia za mkato, watumie mfumo wa E-Huduma kupata cheti halali sababu sisi ndiyo tunaousimamia. Usitumie mtu anakwambia nakutafutia cheti, wengi wanakosa haki za msingi mara baada ya kubainika vyeti si halali.”
Leave a comment