July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

RITA yaita wanafunzi wachukue vyeti

Wanafunzi wa Elimu ya Juu

Spread the love

WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), umewataka wanafunzi wanaojiunga na vyuo vya elimu ya juu, waombe vyeti vya kuzaliwa mapema ili kuepuka usumbufu. Anaandika Mwandishi Wetu …(endelea).

Josephat Kimaro-Meneja Masoko na Mawasiliano kwa Umma, amesema “hivi karibuni wanafunzi wa kidato cha sita wamemaliza mitihani yao. Kumalizika kwa hatua hiyo inaashiria kuanza kwa hatua nyingine ya kuanza kuomba nafasi ya masomo ya elimu ya juu.”

Amesema kutokana na mfumo wa ufadhili wa masomo unaotolewa na Serikali, wanafunzi hao hulazimika kuomba mikopo inayoratibiwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB).

“Katika kuomba nafasi za masomo na mikopo zipo nyaraka mbalimbali zinatakiwa kuambatanishwa na maombi ya mwanafunzi na mojawapo ni cheti cha kuzaliwa. Nyaraka hii huhitajika ili kuthibitisha tarehe na mahali alipozaliwa mwanafunzi.

“Cheti cha kuzaliwa hutolewa na RITA katika ofisi zake za makao makuu na ofisi zilizo katika kila wilaya Tanzania Bara ambazo zipo katika majengo ya ofisi za wakuu wa wilaya,”amesema.

Kimaro amefafanua kuwa kumekuwa na tabia ya wanafunzi wengi kusubiri mpaka tarehe za mwisho za kuwasilisha maombi ndipo wanaanza taratibu za kuwawezesha kupata vyeti vya kuzaliwa, jambo ambalo limewafanya wengi kushindwa kukamilisha taratibu ndani ya muda na hivyo kukosa nafasi za masomo na ufadhili wa serikali.

“Ieleweke kwamba ili kupata cheti cha kuzaliwa zipo taratibu za kisheria lazima zifuatwe ikiwemo kuwa na viambatisho vinavyotambuliwa kisheria, upekuzi ili kujiridhisha kuhusu taarifa mwombaji alizotoa na ada ya cheti.

“Kwa mujibu wa uzoefu wetu, wanafunzi hufika wakiwa hawana viambatanisho au wanakuwa na viambatanisho visivyo sahihi, hivyo kuhitajika kwenda kutafuta vile vinavyokidhi matakwa ya kisheria. Upatikanaji wanyaraka hizo mara nyingi huchukua muda, hivyo kupelekea wanafunzi kutokamilisha taratibu za usajili kwa wakati,”amesema.

Amewasihi wanafunzi, wazazi na wazazi kuanza mchakato wa kupata vyeti vya kuzaliwa sasa ili kuwawezesha kukamilisha taratibu kwa wakati, hivyo kuwa na uhakika wa kupata nafasi za masomo na mikopo.

“Viambatanisho vya msingi vinavyotakiwa wakati wa kuomba cheti cha kuzaliwa ni pamoja naTangazo la kizazi, kadi ya Kliniki, cheti cha kumaliza elimu ya msingi au kidato cha nne, cheti cha ubatizo, cheti cha falaki, pasi ya kusafiria na vinginevyo,” amesema.

error: Content is protected !!