TUME iliyoundwa na Waziri Mkuu, Kasimu Majaliwa kuchunguza mgogoro wa ardhi uliodumu zaidi ya miaka 26 katika vijiji vinavyopakana na hifadhi ya taifa ya Serengeti, imetoa ripoti yake, anaandika Nasra Abdallah.
Akizungumza na waandishi wa Habari Jijini Arusha, Mwenyekiti wa Wilaya ya Ngorongoro, Methew Siloma, amesema pamoja na mambo mengine yaliyopendekezwa na Tume hiyo ya Majaliwa, kitendo cha kutambua kuwa ardhi hiyo ni ya vijiji, Wananchi wa Loliondo wamejenga imani kubwa kwa serikali ya awamu ya tano hasa kwa kupitia ushirikishwaji wa wananchi katika kutafuta suluhu ya kudumu kwa mgogoro huu.
Siloma amesema wamefurahishwa na hatua zote walizopitia kutoka kuanzishwa kwa kamati ya pamoja, mikutano, mrejesho na hatimaye mkutano wa pamoja wa kupata uamuzi wa serikali.
“Viongozi wa vijiji na kata tuliohudhuria katika mkutano wa Waziri Mkuu tumemefurahishwa kusikia serikali ikikiri na kutamka kwamba ardhi ambayo imekuwa ikiingiliwa na Wizara ya maliasili na Utalii na wananchi kupigwa ni ardhi ya vijiji vilivyosajiliwa kisheria na kutambuliwa chini ya mamlaka halali za kisheria.
“Jingine lililotufurahisha ni Tume hiyo kukiri kwamba operesheni iliyoendeshwa mwezi Agosti ilikiuka uadilifu, na kwamba haikuwa agizo rasmi la serikali na hivyo kukosa uhalali wa kisheria.
“Vilevile Waziri Mkuu ametambua kwamba sisi wananchi wa Loliondo ni wahifadhi wa jadi, na kwamba hakuna mgogoro kati yetu na uhifadhi
Kwamba utatuzi wa mgogoro wa maslahi kama huu ni kwa kupitia ushirikishwaji mkubwa wa wadau na kuweka mpango wa pamoja utakaozingatia maslahi ya kila mdau.
“Kwamba Serikali itahakikisha ushirikshwaji wa wananchi kwa kiwango cha juu katika hatua ya kufikia mfumo wa usimamizi wa eneo la ardhi ya vijiji lenye mgogoro,” amesema Mwenyekiti huyo.
Kuhusu maamuzi ya Serikali ya kuunda chombo maalum cha Usimamizi wa ardhi ya vijiji wenye mgogoro uliopendekezwa na tume hiyo, Siloma amesema umeacha maswali mengi ikiwemo namna itakavyoundwa na jukumu lake katika kusimamia maslahi ambayo kwa sasa yanasimamiwa vizuri na kwa uhalali na serikali za vijiji.
Katika hilo, amebainisha kwamba wao viongozi wa jamii kwenye ngazi ya vijiji na kata watakuwa tayari kushiriki katika mchakato huu endapo itazingatia maamuzi yoyote yatakayofanyika hayataathiri Umiliki wa ardhi kwa vijiji ambavyo vipo kisheria.
Huku matumizi halali ya wananchi yataendelea kuwepo na kulindwa kisheria kama ilivyo katika sheria za ardhi na Mpango wa matumizi ya ardhi ya vijiji, upimaji na upatikanaji wa vyeti vya ardhi utafanyika kama hatua ya awali na ya kwanza kabla ya mchakato wowote kufanyika.
Sharti lingine walilolitoa wananchi hawa ni kushirikishwa kikamilifu kutambua mipaka ya vijiji na Hifadhi ya Serengeti kwa njia shirikishi na kuweka alama zilizokubalika kwa pande zote mbili.
“Muda wa kuuweka mfumo wowote unaofikiriwa wa usimamizi wa ardhi, kutengeneza sheria uwe shirikishi na uanzie katika jamii kwa ngazi za vijiji badala ya serikali kuja na mfumo ambao wananchi hawaulewi wala hawaoni kama ni suluhisho la kuleta amani katika eneo hili.
“Pia muda wa majadiliano uongezwe kutoka miezi miwili ya sasa iliyopendekezwa na Waziri Mkuu hadi miaka miwili ili ushirikishwaji wa jamii kwa mapana uweze kufanikiwa,” amweleza Mwenyekiti huyo.
Wakati kwa upande wa wawekezaji, wananchi hao wote kwa pamoja wametaka wawe chini ya jamii ili kuwezesha jamii kunufaika na rasilimali zinazotakana na utalii na kwa zile kanuni zitakazotungwa wametaka zipite kuanzia kwenye ngazi ya vijiji na sio kwa wataalamu wa wizara husika.
Katika hatua nyingine, Siloma alishauri wale wote waliousika na ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Profesa Jumanne Maghembe aliyetoa uamuzi wa kuchomewa maboma kwa wananchi ndani ya ardhi ya kijiji, wachukuliwe hatua za kisheria kwa kuwaumiza wananchi na kuingiza serikali katika mgogoro usio wa lazima na kuchafua taswira ya serikali.
Kwa wale walioathirika na operesheni hiyo, wameiomba serikali iangalie uwezekano wa kutoa fidia kwa wale wote walioathirika na ukiukwaji mkubwa wa haki zao ikiwa ni pamoja na kupoteza mali zao.
Leave a comment