Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Ripoti ya CAG, mtihani mzito
Habari za SiasaTangulizi

Ripoti ya CAG, mtihani mzito

Prof. Mussa Assad, aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali
Spread the love

RIPOTI ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ipo njia moja kuelekea Bunge la Jamhuri ya Muungano, lakini je, itafikishwa? Na ikifikishwa itasomwa? Halafu ikishasomwa? Anaandika Bupe Mwakiteleko…(endelea).

Ripoti hiyo ipo kwenye kituo cha kwanza (kwa Rais John Magufuli), kituo chake cha pili ni bungeni. Lakini ripoti hiyo imeandaliwa na Prof. Mussa Assad, mkuu wa taasisi hiyo (CAG) ambaye bunge limegoma kufanya kazi naye.

Hapa ndio hoja ya Dk. Benson Bagonza, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Doyosisi ya Karagwe inaibuka kwamba, kama Rais Magufuli ataipeleka ripoti hiyo bungeni, atakuwa amelipuuza Bunge na kama hatoipeleka atakuwa amevunja Katiba ya Nchi. Tusubiri.

Prof. Assad anatambua hilo, naye tayari ametoa tahadhari kwamba, mgogoro unaweza kuwa mkubwa kutokana na uamuzi wa Bunge kumtenga huku ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2017/18 ikiwa tayari imeandaliwa.

Ndani ya siku saba, baada ya bunge kuanza kuketi tarehe 2 Aprili 2019, ripoti hiyo inapaswa kufikishwa bungeni na kusomwa.

Job Ndugai, Spika wa Bunge jana tarehe 4 Aprili 2019 amesema kuwa, Ripoti ya CAG ya mwaka 2017/18 haijafika mikononi mwake, kwa lugha nyingine ni kwamba, bado ipo Ikulu.

Ni kwa kuwa, Prof. Assad alisema tayari ameshaikabidhi ripoti hiyo kwa Rais Magufuli na kwamba, kinachosubiriwa kwa sasa ni kuwasilishwa bungeni kama inavyoelekezwa na Katiba na sheria za nchi.

Ni kwa mujivu wa Ibara ya 143(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 ambapo inamtaka CAG kuwasilisha kwa Rais kila taarifa atakayotoa.

Kwa mujibu wa ibara hiyo, baada ya rais kupokea taarifa hiyo, atawaagiza watu wanaohusika wawasilishe taarifa hiyo kwenye mkutano wa kwanza wa Bunge, utakaofanyika baada ya rais kupokea taarifa hiyo.

Na kuwa, ripoti hiyo itapaswa iwasilishwe katika mkutano huo kabla ya kupita siku saba tangu siku kikao cha bunge kilipoanza.

Maana yake ni kwamba, ripoti ya CAG inapaswa kuwasilishwa bungeni kabla ya Alhamisi ya wiki ijayo.

Spika Ndugai alikutana na waandishi wa habari jana ambapo miongoni mwa maswali aliyoulizwa, ni kwamba, ameishapokea ripoti ya CAG ya mwaka 2017/18 iliyosainiwa na Prof. Assad?

“Bado” ndivyo alivyojibu na kwamba, haoni sababu ya kueleza kama mhimili huo wa kutunga sheria utapokea ripoti hiyo na kuifanyia kazi ama la!

Hata hivyo Spika Ndugai alisisitiza kwamba, Bunge halifanyi kazi na Prof. Assad na kwamba,halijakataa kufanya kazi na Ofisi ya CAG.

Spika Ndugai anasema, walikwazwa kwa kauli ya Prof. Assad kwamba, Bunge ni dhaifu wakati Bunge hilo ndio linashirikiana naye kwa kiwango kikubwa na ofisi yake inashiriki katika utekelezaji wa shughuli za chombo hicho cha kutunga sheria.

Jumanne wiki hii, Bunge lilipitisha azimio la kutofanya kazi na Prof. Assad baada ya Kamati yake ya Kudumu ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuwasilisha taarifa kuhusu shauri dhidi yake kwamba, alilidharau bunge.

Lakini je, Ripoti ya Ukaguzi ya mwaka 2017/18 iliyosainiwa na Prof. Assad itafikishwa bungeni? Itafanyiwa kazi na Bunge licha ya kutangaza kumtenga?

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!