Thursday , 18 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa CAG awavua nguo tena Chadema, CCM
Habari za SiasaTangulizi

CAG awavua nguo tena Chadema, CCM

Spread the love

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad, ameibua tuhuma za kuwapo kwa matumizi mabaya ya madaraka ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, leo tarehe 10 Aprili, Prof. Assad amesema, vyama hivyo viwili na vingine saba, vimefanya makossa makubwa ya kihasibu, yanayoweza kuingiza taifa katika hasara ya mabilioni ya shilingi.

Akichambua chama kimoja baada ya kingine, Prof. Assad amesema, Chadema kimenunua gari aina ya Nissan Patrol, kinyume cha taratibu za manunuzi na baadaye kutaka kuliondoa kwenye umiliki wa chama, kinyume na taratibu.

Katika taarifa yake hiyo, Prof. Assad amesema, “tarehe 30 Machi 2017, Bodi ya wadhamini ya Chadema, iliingia mkataba ya AMC Tanzania Limited kwa ajili ya ununuzi wa gari jipya aina ya Nissan Patrol Y61 – GRX kwa bei ya dola za Kimarekani 63,720 (Sh. 147,760,080).”

Anasema, kifungu cha 1 cha Mkataba huo, kinaelekeza kuwa gari hilo litakalonunuliwa, lisajiliwe kwa jina la Bodi ya Wadhamini ya chama hicho.

Hata hivyo, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu huyo wa fedha za Serikali anasema, “kinyume na masharti yaliyomo kwenye mkataba, Ibara ya 1, gari hilo lilisajiliwa kwa jina la mbunge.”

Anasema, “hata baada ya kupitia rejesta ya mali za chama, nilibaini kuwa hakuna kumbukumbu za gari aina ya Nissan Patrol, Y61 -GRX, lililosajiliwa kwenye rejesta za mali ya Chadema, pamoja na gari hilo kununuliwa na fedha za chama na kutumika na Chadema.”

Anaongeza, “zaidi ya hayo, gari lililonunuliwa liliingizwa kwenye taarifa za fedha za chama kama mkopo, uliotolewa kwa mbunge bila makubaliano yoyote kati ya mbunge na Bodi ya Wadhamini ya Chadema.

“Nilibaini kuwapo kwa mawasiliano ya barua kati ya mbunge na Chadema kuhusu kusitishwa kwa mkataba wa mkopo na urejeshwaji wa gari hilo. Jambo hili lilitokea, mapema tu, baada ya kutoa hoja ya ukaguzi,” anaeleza Prof. Assad.

Anasema,“hata hivyo, wakati wa ukaguzi wangu, Februari 2019, mkataba wa mkopo huo, haukuwasilishwa kwa ajili ya ukaguzi. Kwa maoni yangu, ni kwamba kuonyesha thamani ya gari kama mkopo kwa mbunge, kunapotosha watumiaji wa taarifa za fedha za chama.”

Kutokana na hali hiyo, CAG ameelekeza kuwa usajili wa gari hilo aina ya Nissan Patrol Y61-GRX yenye rangi nyeupe, “ufanyike kwa jina la mmiliki ambaye ni Bodi ya Wadhamini ya Chadema na deni hilo la takribani Sh. 150 milioni, liondolewe kwenye taarifa za fedha za chama.”

Haya yanajiri, katika kipindi ambacho Chadema kimeshindwa kujibu kwa ufasaha, madai ya CAG yam waka uliyopita, ambako chama hicho kilidaiwa kuwa kimetengeneza “madeni hewa na makusanyo yasiyoingizwa kwenye akaunti zake.”

Katika ripoti yake yam waka uliopita, CAG ameeleza katika ukurasa 266, kuwa chama hicho kilidai kupokea mkopo wa Sh. 866 milioni kutoka kwa mmoja wa wanachama wake; mkopo huo haukuthibitishwa na bodi ya wadhamini wala kupokelewa wake.

Fedha hizo zilidaiwa kulipwa kwa mwanachama huyo kwa niaba ya chama nje ya deni hilo, kwa ajili ya mabango na Sh765 milioni zililipwa kwa mwanachama kama marejesho ya fedha hizo bila kuambatanisha makubaliano ya kisheria.

Kwa upande wa CCM, Prof. Assad amesema, ofisi yake imebaini kuwa hakikuwasilisha michango yake ya wafanyakazi ya kila mwezi kwa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Anasema, hadi kufikia Mei mwaka 2018, Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), ulikuwa unadaiwa zaidi ya Sh. 3,741,358,870.97 ikiwemo deni la adhabu lililotokana na ucheleweshaji wa uwasilishaji michango yake.

Aidha, umoja huo umesababisha hasara ya zaidi ya Sh. 230 milioni, kwa kutokuwepo kwa mkataba mpya wa ukodishaji ardhi na Kampuni ya Manji Holdings Limited kwa ajili ya uendelezaji wa jengo la ‘ZANRAN TOWER’.

“Mbali na hilo, nimebaini kuwa UWT (CCM) uliingia mkataba na mwekezaji Manji Holdings Limited kwa kukodisha ardhi kwa ajili ya uendelezaji wa jengo. Hatahivyo, hakukuwa na mkataba mpya kwa ajili ya kukodisha jengo na kusababisha hasara ya kiasi cha Sh. 230,000,000 pamoja na ada ya ucheleweshaji wa malipo ya asilimia 10 kwa mwaka,” inaeleza ripoti hiyo.

Ripoti hiyo inasema, hati za ardhi za nyumba 199 zinazomilikiwa na CCM Zanzibar, katika ukaguzi zilionekana hazijasajiliwa kwa jina la Bodi ya Wadhamini ya chama hicho, badala yake zimesajiliwa kwa majina ya maafisa wa chama hicho.

Anasema, “…nilibaini kuwa CCM kilishindwa kukusanya Sh. 1,457,173,050 hadi mwezi Juni, 2018. Kwa upande mwingine nimebaini kuwapo kwa manunuzi ya gharama za uchapishaji yanayofikia Sh. 524,777,538 yaliyofanywa na Kampuni ya Uchapishaji ya Uhuru bila kufuata taratibu za manunuzi.”

Mbali na CCM na Chadema, CAG amevitaja vyama vingine vitatu – United Democraty Party (UDP), UPDP, Chama cha Kijamii (CKK) na ADA-TADEA – kuwa havikuwa na rejista ya maelezo ya mali.

Vyama vingine saba, vimeelezwa kufanya matumizi ya Sh 777,910,739.72 bila ya kuwa na nyaraka toshelezi.

“Hivyo nilishindwa kuthibitisha kama malipo hayo yalikuwa halali, na kama yalihusiana na shughuli za vyama vya siasa.

“Zaidi, nimebaini kuwa, CCM, CHADEMA, na ACT-Wazalendo havikudai na kutunza risiti za kielektroniki kwa kiwango kinachofikia Sh. 85,186,705,” inaeleza sehemu ya ripoti ya CAG.

Katika ripoti hiyo, vyama 11 vyama vine vilipata hati yenye shaka, vitano vilipata hati mbaya huku vyama wivili vikipata hati isiyoridhisha.

Kwa mujibu wa ripoti ya CAG iliyotolewa leo tarehe 10 Aprili 2019 katika tovuti ofisi yake, ukaguzi huo ulibaini taarifa za fedha za vyama hivyo zilikuwa na dosari katika miamala ya fedha.

“Matokeo ya vyama vya siasa kwa taarifa za fedha za mwaka 2017/18 yanaonesha kwamba, vyama vya siasa 14 vilikaguliwa, 3 (21%) vilipata hati zinazoridhisha, 4 (29%) vilipata hati yenye shaka, 5 (36%) vilipata hati mbaya na 2 (14%) vilipata hati isiyoridhisha.

“Hii inamaanisha kuwa, taarifa za fedha za vyama vya siasa zilikuwa na dosari katika miamala ya fedha,” imeeleza ripoti ya CAG.

Pia, ukaguzi huo umebaini vyama vitano, ikiwemo CCM, UDP, UPDP, CKK na ADA-TADEA havikuwa na rejista ya maelezo ya mali, huku vyama saba vikifanya matumizi ya Sh. 777,910,739.72 bila ya kuwa na nyaraka toshelezi.

Ripoti hiyo kuwa, Chadema  kilinunua magari yenye thamani ya zaidi ya Sh. 172 bilioni pasipo kuwa na nyaraka na au uthibitisho wa kupokelewa hadi wakati wa ukaguzi wa mwezi Januari mwaka huu.

Aidha. Ripoti hiyo imebainisha kwamba, vyama vya CCM, CHADEMA na ACT-Wazalendo havikudai na kutunza risiti za kielektroniki kwa kiwnago kinachofikia Sh. 85,186,705.

“Pia, nimebaini kuwa SAU hakijateua bodi ya wadhamini vile vile taarifa za fedha kutoka SAU, UPDP, UMD , ADA-TADEA, NLD na AAFP zilikuwa haziendani na mwongozo wa mfumo dhanifu wa viwango vya kimataifa vya uandaaji wa hesabu za umma, Kadhalika, bakaa la madeni yanayofikia Sh. 85,366,000 yaliyoelezwa kwenye taarifa za fedha za NCCR-Mageuzi hayakuwa na nyaraka za kuyathibitisha.

Kufuatia dosari hizo zilizojitokeza kwenye ukaguzi wa CAG, Prof. Assad amependekeza vyama vya siasa kuhakikisha udhibiti unaanzishwa na kuimarishwa hasa kwenye malipo ili yote yawe na vielelezo na nyaraka toshelezi, zikiwamo risiti za kielektroniki.

“Aidha, viboreshe utunzaji wa nyaraka kwa muda unaotakiwa kama ilivyoelezwa kwenye kanuni za fedha za vyama husika,” amependekeza Prof. Assad.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza ajira watendaji daftari wapiga kura

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza nafasi...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

Habari za Siasa

CCM yamkana mwenyekiti UVCCM aliyetaka wapinzani wapotezwe

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimejitenga na kauli ya mwenyekiti...

error: Content is protected !!