Spread the love

 

IMEELEZWA kuwa asilimia kubwa ya viongozi wa ngazi mbalimbali nchini hawana utamaduni wa kuwa karibu na wananchi jambo linalowafanya washindwe kutambua mahitaji halisi ya wananchi wanaowaongoza.

Hayo yamebainishwa leo tarehe 19 Januari , 2022 na Taasisi ya Mwalimu Nyerere katika ripoti ya majumuisho ya midahahalo iliyokuwa ikijadiliwa na wadau mbalimbali kwa lengo la kujadili masuala ya utaifa. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Katika taarifa hiyo maoni mbalimbali yaliyotolewa na wadau yameingizwa katika ripoti hiyo kwa lengo la kuyatafutia ufumbuzi.

Akiwasilisha taarifa kwa wadau wa Taasisi hiyo ya Mwalimu Nyerere, Prof. Francis Matambalya amesema katika baadhi ya maoni ambayo yalitolewa na wadau ni pamoja na viongozi kutokuwa karibu na wananchi.

Amesema baadhi ya wananchi waliotoa maoni yao walisema viongozi hawana utamaduni wa kuwa karibu na wananchi hivyo kushindwa kujua mahitaji halisi ya wananchi wanaowaongoza.

Prof. Matambalya amesema baadhi ya wadau waliotoa maoni yao walisema kuwa ili kuboresha utendaji wa kazi hususani kwa nafasi ya ubunge wanatakiwa kuwepo kwa watafiti ili kuwawezesha kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Amesema imeonesha kuwa wabunge wengi wanashindwa kufanya kazi vizuri kutokana na kutokuwa na utafiti wa kina kutokana na kushindwa kuwa na utafiti unaostahili.

Katika hatua nyingine Prof. Matambalya amesema kuna haja ya kuimarisha umoja, udugu na ushirikiano pamoja na uimarishaji ya mifumo kwa kuacha kila muhimili kufanya kazi yake kwa misingi ya kisheria, kanuni na taratibu.

Aidha, katika taarifa hiyo yamo mapendekezo ambayo yametaka vyombo vya dola kama vile polisi kutoegamia upande mmoja na badala yake watende haki kwa vyama vyote vya siasa na wanasiasa.

Aidha, ripoti hiyo imekuwa na mapendekezo ya kuwepo kwa katiba mpya, tume huru ya uchaguzi, pamoja na majadiliano ya maridhiano ya kitaifa.

Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Joseph Butiku amesema waliandaa mdahalo wa kitaifa ambao mada yake ilikuwa ikisema; “Tushirikiane kudumisha na Kuimarisha Udugu, Uzalendo, Uwajibikaji, Amani, Maridhiano na Maendeleo yetu.”

Akizungumza na wadau wa taasisi ya hiyo, Butiku amesema mdahalo huo ni sehemu ya mradi mkubwa unaohusu “Umuhimu wa Kujali, Kuzingatia na Kulinda Amani na Demokrasia Nchini kwa Mujibu wa Katiba na Sheria.”

“Mradi huu unatakelezwa kwa kuwashirikisha wadau wa Amani na Demokrasia, ambao ni pamoja na wananchi na viongozi wa vyama vya siasa, jumuia za vyama hasa vijana, viongozi wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.

“Viongozi wa dini na asasi za kiraia ili kujadili na kutoa maoni yao kuhusu umuhimu wa kujali na kuimarisha umoja, amani na kulinda demokrasia kwa kuzingatia Katiba na Sheria” ameeleza Mwenyeki.

Aidha, amesema lengo kuu la mdahalo huo ni kusisitiza viongozi na wananchi ndio wadau wakubwa katika kufanikisha suala la kulinda na kuimarisha Umoja, Amani, Mshikamano wa Kitaifa, Demokrasia, Katiba na Sheria za Nchi.

“Mdahalo huo umetanguliwa na midahalo na mashauriano na viongozi wa serikali, vyama vya siasa na jumuia zake, viongozi wa dini na taasisi zinazoshughulikia uchaguzi.

“Pia taasisi za ulinzi na amani, vyombo vya habari, asasi za kiraia na taasisi za utawala bora, iliyofanyika kati ya miezi ya Septemba na Novemba 2021Tanzania Bara na Zanzibar katika miji ya Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *