January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Richmond ilimzamisha Sitta, bado BMK

Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta

Spread the love

RASHID Mfaume Kawawa “Simba wa Vita” ni miongoni mwa viongozi waliotaniwa sana nchini. Kutokana na ufupi wake gia fupi itumikayo kuongeza nguvu katika gari iliitwa Kawawa.

Vilevile, alitaniwa kutokana na historia yake ya kuigiza filamu kadhaa ikiwemo maarufu ya “Mhogo mchungu.” Pamoja na utani huo ambao ni afya katika jamii, Kawawa alikuwa kiongozi madhubuti aliyelitumikia taifa hili kwa uzalendo na uadilifu

Kawawa aliwahi kuongoza taifa kama Waziri Mkuu baada ya Mwalimu Julius Nyerere kujiuzulu. Baada ya Katiba kurekebishwa awepo rais, Kawawa aliteuliwa katika nafasi tofauti, waziri mkuu, waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga taifa na waziri asiye na wizara maalum.

Kawawa ametangulia mbele za haki lakini huwezi kuzungumzia vita dhidi ya nduli Idi Amin Dada bila kumtaja pamoja na mafanikio mengi mengine. Ni katika vita ile (1978 – 1979) Kawawa aliitwa Simba wa Vita.

Mwalimu Nyerere, wakati wa mapumziko ama alicheza bao pamoja na wazee wengine na kuna wakati alichezesha mechi kati ya mawaziri na wabunge. Kwa hiyo, usanii na uchezaji ni fani tu ambazo hazimzuii mtu kuibuka na kuwa kiongozi madhubuti wa kisiasa.

Nimeeleza haya kumfahamisha Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM) na Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba (BMK), Samwel Sitta kwamba hakuna mtu aliyeumbwa kuwa msanii, mwigizaji, mchezaji, mchezaji asiyekuwa na maana katika jamii. Hizo ni fani tu.

Ni muhimu Sitta akalijua hili kwamba mtu anaweza kuwa msanii na mwanasiasa mzuri; au mchezaji na mwanasiasa mzuri. Inasikitisha kuona mwanasiasa wa aina yake anasema wapinzani ni wachekeshaji ambao wakishindwa katika uchaguzi mkuu ujao watarejea kwenye fani yao.

Kwani wasanii hawana akili? Nani kasema wasanii hawajasoma hivyo hawawezi kuaminiwa kazi za kisiasa? Mbona wasanii kama John Komba, Vick Kamata, Martha Mlata (wote CCM) na Joseph Mbilinyi (Chadema) ni wasanii na ni wabunge?

Sitta anajua Ronald Reagan alikuwa msanii lakini alikuja kuwa Rais wa Marekani mwenye nguvu duniani. Pia anajua katika miaka ya hivi karibuni Jimbo la California lilimchagua mwigizaji wa filamu Arnold Alois Schwarzenegger mzaliwa wa Austria kuwa gavana lakini anadai haujafika wakati Afrika na hasa Tanzania kuwa na viongozi wa fani ya uchekeshaji.

Sitta hajui asemalo. Kabla ya kuukwaa urais wa Madagascar mwaka 2009, Andry Rajoelina alikuwa DJ maarufu wa kituo cha televisheni cha familia yao katika Jiji la Antananarivo. Mwaka 2007 akawa meya wa jiji.

Akiwa meya, Rajoelina alitumia nafasi hiyo kupinga sera za uchumi za Rais Marc Ravalomanana, na baada ya serikali kuamua kuifunga TV yake Desemba 2008, aliongoza maandamano mazito. Huku akiungwa mkono na Jeshi la Madagascar, Rajoelina alimng’oa Ravalomanana na akaongoza nchi hiyo hadi mwaka jana ulipofanyika uchaguzi mkuu na kumweka madarakani Hery Rajaonarimampianina.

Sidhani kama Sitta ni msahaulifu! Kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 kuna wanasiasa wawili nchini walifurahia kuitwa Boyz II Men jina la kundi la wasanii wa Marekani. Waliofurahia jina hilo lenye maana ya wavulana wanaokua kuwa wanaume, hawakuwa wengine bali Jakaya Kikwete na swahiba wake Edward Lowassa.

Baada ya Kikwete kuukwaa urais hakutaka tena kuitwa kwa jina hilo la wasanii wa Marekani. Hata hivyo, alipokwenda Marekani Rais Kikwete alipiga picha na wasanii wa kundi hilo, msanii maarufu wa sinema Steven Siege, na wengineo wengi.

Nasikia Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa kwanza wa Zanzibar, alipiga marufuku mchezo wa ngumi katika visiwa hivyo kwa maelezo vijana wanaharibika akili. Lakini nchi nyingine, kuna mabondia waliokuja kuwa marais

Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, Nelson Mandela aliwahi kuwa bondia, Theodore “T.R.” Roosevelt, Jr rais wa 26 wa Marekani pia alikuwa bondia na hivi sasa ikulu ya Kremlin, Urusi kuna mcheza kung’fu anaitwa Vladimir Putin.

Sitta, alikuwa mtu wa kwanza kuonesha nia ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2015. Mara ya kwanza ilikuwa alipokuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Waandishi wa Habari 2012 na mara ya pili ni mwaka jana aliposhiriki Kongamamo la Mawasiliano katika Nyanja za Digitali la wanafunzi wa Idara ya Uhusiano na Masoko, Chuo Kikuu cha St. Augustine (SAUT), Mwanza.

Sitta alisema wakati ukifika, yeye na rafiki zake Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, watachagua mmoja wao watakayeona anafaa kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Hao aliowaita marafiki haraka walimkana Sitta. Membe, mmoja wa wanasiasa waliofunguliwa mafaili kwa kosa la kuanza kampeni kwa siri, hupenda kudai anasubiri kuoteshwa agombee kiti hicho cha enzi.

Mgufuli pamoja na Mwakyembe ambaye alikuwa mshirika mkuu wa Sitta katika sakata la ufisadi wa Richmond, alikanusha kuwemo katika mpango huo.

Sitta alisema yeye na rafiki zake hao wana mawazo yanayolingana katika mustakabali wa nchi hii na kwamba wataendelea kutembea sehemu mbalimbali za nchi kuwajengea wananchi uelewa ili wajue kuwa uongozi ni lazima ukae katika mikono salama.

Hivyo, Sitta alipoteuliwa kuwa Mwenyekiti wa BMK aliona ni kete muhimu ya kumjenga akionesha alivyo madhubuti katika kusimamia mambo muhimu yenye maslahi kwa taifa kwa umakini, uadilifu na ujasiri.

Sitta ajue ana kazi pevu. Kwanza wale jamaa aliodai walimhujumu katika nafasi ya uspika walipompa sharti la kuotesha matiti au aliowaudhi aliposhupalia suala la Richmond ndio wamesimama katika njia ya urais anaotaka. Pili ni madudu anayofanya katika BMK.

Makala haya imeandikwa na Joster Mwangulumbi

error: Content is protected !!