December 8, 2021

Uhuru hauna Mipaka

RC Ruvuma ameshindwa kuwajibisha wezi Mbinga

Spread the love

GAZETI la Nipashe Jumapili tarehe 27 Julai mwaka jana, lilibeba ujumbe mzito, ulioandikwa na Gideon Mwakanosya, kutoka Songea mkoani Ruvuma, kwamba “Mkuu wa mkoa wa Ruvuma (RC), ameahidi kuwashughulikia watakaohujumu wilaya ya Mbinga.”

Nikiwa mwenyeji wa Mbinga, habari hii kwangu ni nzito na inastahili kupongezwa hata kama imechelewa kuandikwa, hasa kutokana na maslahi ya wananchi wa wilaya hii, wanaoteseka na umaskini.

Ninampongeza pia mwandishi wa habari hiyo, Mwakanosya kwa ujasiri wake. Hii ni kwa sababu, wakuu wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliowengi kutoka mkoani Ruvuma na hasa wilaya ya Mbinga, hawapendi maandishi kama hayo.

Huu ni mwanzo mzuri wa kuleta mwanga katika jamii ya Wanambinga ambayo ina njaa ya kusikia ukweli wa matukio yanayotokea katika wilaya yao hususani maovu yaliyojikita ndani ya halmashauri.

Wilaya ya Mbinga ni kati ya wilaya tajiri nchini. Lakini ni ya mwisho kwa maendeleo kutokana ukosefu wa uongozi bora serikalini na jamii. Wananchi wa Mbinga ni watendaji sana lakini wanaangushwa na viongozi.

Wilaya ya Mbinga haijawahi kupata viongozi wenye uchungu; kila anayekuja hapa huishia kujinufaisha binafsi. Ni kama “shamba la bibi.” Wilaya ya Mbinga ina mapato mazuri sana, lakini kumesheheni ubadhirifu.

Halmashauri ya Mbinga, imepata hati chafu mara nne mfululizo; hoja 37 zilizoelekezwa na Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za serikali, bado hazijajibiwa.

Wakati haya yanafanyika, viongozi wa CCM wanasema, “Mbinga ni hazina ya kura za CCM.” Ni ujasiri wa hali ya juu kuendelea kuchagua chama ambacho kipo mbali na wananchi.

Naye mkuu wa mkoa wa Ruvuma ameshindwa kuwawajibisha wabadhirifu (wezi) wa rasilimali za wilaya ya Mbinga. Je, nani atafanya kazi hiyo? Yako wapi maisha bora kwa kila Mtanzania ambayo mmeahidiwa na Rais Jakaya Kikwete mwaka 2005? Hakuna. Kinachoonekana, ni wizi mtupu.

Mwandishi wa Makala hii ni Padre Baptiste Mapunda anapatikana kwa  frmapunda91@gmail.com

error: Content is protected !!