May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

RC Mtaka: Napokea malalamiko 130 ya ardhi kila siku

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma (RC), Anthony Mtaka

Spread the love

 

MKUU wa Mkoa wa Dodoma (RC), Anthony Mtaka amesema, kwa kipindi cha siku 30 alizoanza kufanya kazi katika ofisi hiyo, amekuwa akipokea wananchi kati ya 100 hadi 130 kwa siku wenye malalamiko ya ardhi. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Mtaka, ametoa taarifa hiyo kwenye kikao cha Willium Lukuvi, Waziri wa Ardhi, mkuu wa mkoa, viongozi wa chama, viongozi wa mabaraza ya ardhi na wataalamu wa ardhi kilichofanyika jana Ijumaa, tarehe 2 Julai 2021, ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkoa wa Mkoa wa Dodoma.

RC Mtaka aliyehamishiwa mkoani humo hivi karibuni kutoka Simiyu amesema, Dodoma pamoja na kupewa hadhi ya kuwa makao makuu, bado kuna changamoto kubwa ya migogoro ya ardhi ambayo inatakiwa kutatuliwa.

“Tangu nimeingia ofisini kwa muda wa siku 30, ofisini kwangu nimekuwa nikipokea wananchi wenye malalamiko ya ardhi kati ya 100 hadi 130 kwa siku jambo ambalo ni tatizo kubwa kwa jamii.”

“Nimeona kuwa haiwezi kuwa jambo jema jiji la Dodoma kuwa na sehemu ya migogoro kwani ikiwepo migogoro ya ardhi isiyoisha hatuwezi kuwa na maendeleo kama inavyotakiwa,” amesema.

“Kwa hali hiyo, nimeona ni vyema kuitisha kikao ili kuweza kujadili jambo hili na kulitafutia ufumbuzi na ufumbuzi wenyewe tumepanga kutumia ukumbi wa Jakaya Kikwete kwa siku tatu kusikiliza kero za watu wenye migogoro ya ardhi wakiwa na nyaraka zao.

“Lakini pia, tutatumia siku saba kwa ajili ya kutembelea kata zote 41 ili kubaini ni kata ipi inaongoza kwa kuwa na migogoro kwa lengo la kuhakikisha tunakuwa na Dodoma Jiji isiyokuwa na migogoro,” amesema Mtaka.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi

Katika hatua nyingine, Mtaka baada ya kumaliza kushughulikia migogoro katika Jiji la Dodoma, ataanza kutembelea wilaya zote ili nazo ziweze kubaini niwapi kuna migogoro na jinsi ya kuitatua.

“Nia ni kuona Dodoma ambapo wanaishi viongozi, Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na viongozi wengine panakuwa sehemu ambayo haina migogoro na kuwepo na utulivu.”

Naye Waziri Lukuvi katika Kikao hicho alisema, anatoa agizo kwa wakuu wote wa mikoa na wakuu wa wilaya kuwa na madaftari yanayobainisha kiwango cha migogoro ya ardhi katika eneo husika ili kupata wepesi wa kuitatua.

Jambo lingine ambalo Lukuvi alilisema, ni marufuku kwa watendaji wote wa mitaa iliyopo mijini kuuza maeneo.

“Nimetoa maagizo kwa watendaji wote wa mitaa kujiepusha na uuzaji wa maeneo kwani mwenye mamlaka hiyo ni mkurugenzi wa halmashauri husika, pamoja na hilo mtu yeyote anayetaka kununua maeneo ni lazima ajiridhishe kwa mkurugenzi kama kweli eneo ni sahihi au la.”

“Tumekuwa tukipokea malalamiko ya watu ambao wananunua maeneo ambayo si sahihi na hii inatokana na tatizo la kutofuata utaratibu ambao unatakiwa kufuatwa” ameeleza Lukuvi.

error: Content is protected !!