ANNA Elisha Mghwira, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro (RC),nchini Tanzania, amewashukuru wananchi wa mkoa huo akisema “nitawakumbuka daima.” Anaripoti Mwandishi Wetu, Kilimanjaro … (endelea).
Ametoa shukurani hizo, leo Jumapili tarehe 16 Mei 2021, ikiwa ni siku moja imepita, tangu Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alipoteua wakuu wa mikoa akiwemo wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai.
Kagaigai, aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanzania, anachukua nafasi ya Mama Mghwira, ambaye amestaafu. Kwa sasa ana miaka 62. Alizaliwa tarehe 23 Januari 1959, mkoani Si ngida
Katika ukurasa wake wa Facebook, Mama Mghwira ameandika “Asanteni sana Kilimanjaro.”
“Ninamshukuru Mungu kwa muda wote nilioishi na kufanya kazi Kilimanjaro. Asanteni kwa ushirikiano na mshikamano.”
“Tuendeleze umoja huu na nguvu ya pamoja kwa masilahi ya mkoa na taifa. Nitawakumbuka daima. Mungu awape kila mmoja hitaji la moyo wake,” amesema Mama Mghwira
Mama Mghwira, aliteuliwa kuwa mkuu wa mkoa huo na aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Pombe Magufuli, tarehe 3 Juni 2017, ikiwa ni takribani miaka miwili imepita tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015.
Katika uchaguzi huo, Mama Mghwira, alikuwa mgombea urais kupitia chama cha ACT-Wazalendo, akichuana na Hayati Magufuli na wagombea wengine. Hata hivyo, Magufuli aliibuka mshindi kwenye uchaguzi huo.
Wakati akiteuliwa kuwa mkuu wa mkoa, kuchukua nafasi iliyokuwa imeachwa wazi na Said Meck Sadiki, Mama Mghwira, alikuwa Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo.

Ujumbe huo wa kuwashukuru wana Kilimanajro, umepongezwa na watu mbalimbali, wakimpongeza kwa utumishi wake uliotukuta.
Shoumar B’van Mbwana amesema “niliiona nia yako nzuri kwa Watanzania tangu mwaka 2015 uliposimama kuwania kiti cha urais kwa tiketi ya ACT Wazalendo ukiwa mwanamke pekee uliyewania kiti hicho.”
“Na sasa umemaliza utumishi wako, Kilimanjaro ila bado unaweza kuendelea kufanya kitu kwa Kilimanjaro yenyewe na hata kwa Watanzania. Hongera.”
Leave a comment