August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

RC Makalla aishangaa Serikali kuu

Spread the love

AMOS Makalla, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, ameshangazwa na hatua ya serikali kuu kupeleka fedha Sh. 9.6 bilioni kwa uongozi wa Chuo cha Ualimu cha Mpuguso kilichopo wilayani Rungwe bila kutoa taarifa kwa uongozi wa mkoa, anaandika Esther Macha.

Serikali imetoa Sh. 9.6 bilioni kwa uongozi wa chuo cha Mpuguso kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya chuo hicho kilichopo wilayani Rungwe mkoani Mbeya, kilichoanzishwa mwaka 1975 huku miundombinu yake ikiwa chakavu na isiyokidhi mahitaji.

Fedha hizo zitatumika kujenga nyumba 13 za watumishi, madarasa 6, mabweni mawili, ukumbi wa mikutano , ukumbi wa mihadhara, maabara za sayansi mbili, maktaba pamoja na vyoo.

“Uongozi wa chuo hiki muhakikishe mnatumia fedha vizuri na majengo yanayojengwa yawe yenye ubora kulingana na fedha iliyotolewa na serikali,” amesema Makalla.

Aidha Makalla amesema hatua ya Serikali kuu kupeleka fedha hizo mkoani Mbeya bila ya kuutarifu uongozi wa mkoa si mzuri kwani fedha hizo ni nyingi na zinahitaji usimamizi mkali.

“Pamoja na nia nzuri ya serikali ya kuleta fedha hizo ambazo ni nyingi lakini mkoa na wilaya haukupewa taarifa ya serikali kuu kuleta fedha hizo. Mkoa na wilaya lazima zisimamie vyema matumizi ya  fedha hizo kama viongozi wakuu  na wasimamizi wa shughuli zote.

Ni vizuri Serikali kuu iwe inatoa taarifa kwa mkoa  na wilaya pale  zinapoletwa fedha kwani fedha hizo ni nyingi na mradi ni  mkubwa  hivyo kunahitajika uangalizi mkubwa,” amesema.

Doroth Mhaiki, Mkuu wa chuo hicho amesema ukarabati na ujenzi mpya chuoni hapo utaboresha makazi ya wakufunzi na kuongeza morali ya utendaji kazi kwa wakufunzi.

“Katika mradi huu mkubwa unaoendelea, zaidi ya wananchi 100 waliopo wilayani hapa wameweza kunufaika na ajira za muda mfupi kutoka kwa makampuni yanayojenga majengo ya chuo chetu,” amesema Mhaiki.

error: Content is protected !!