August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

RC: Machinga lazima waondoke

Polisi akipambana na wamachinga katika jijini Mwanza

Spread the love

JOHN Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza amesema kuwa, mpango wa kuwaondoa wafanyabiashara ndogo ndogo (Machinga) katikati ya Jiji la Mwanza upo pale pale, anaandika Moses Mseti.

Tarehe 3 Desemba, mwaka huu wakuu wa wilaya mbili za Nyamana na Ilemela, walianza kutelekeza agizo la Mongella la kuwaondoa machinga kutoka katikati ya jiji kabla ya Rais John Magufuli kuagiza kuchwa waendelee na shughuli zao kama kawaida.

Mongella ametoa kauli hiyo leo wakati wa kikao cha pili cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Mwanza (RRB) kilichofanyika katika ofisi za mkuu wa mkoa huo.

Kikao cha Bodi ya Barabara kilichofanyika tarehe 28 Julai mwaka huu kilizungumzia suala la machinga kuondolewa katikati ya jiji lakini washiriki wa kikao hicho waliazimia wafanyabiashara hao watengewe maeneo ambayo ni rafiki kwa shughuli zao.

Mongella amesema kuwa, zoezi la kuwaondoa wafanyabiashara hao lililositishwa na rais Magufuli tarehe 6 Desemba mwaka huu, limetafsiriwa vibaya na Wananchi kwamba, machinga wanafukuzwa mjini.

Mongella amelamizimika kuzungumzia suala hilo baada ya hoja iliyoibuliwa na John Wanga, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela kumuomba mwenyekiti wa kikao hicho (Mongella) suala la machinga lizungumziwe.

“Hilo suala tayari lilishatolewa maelekezo kutoka juu, lakini kama mnataka tulizungumzie ni kwamba watu wanatafsiri vibaya kuondolewa kwa machinga, hatuwafukuzi bali ni utaratibu wa kupanga na kusafirisha jiji,” amesema Mongella.

Mongella amesema kuwa, zoezi la kuwaondoa machinga hao bado lipo pale pale na kwamba, watawaondoa baada ya kuwatafutia maeneo ambayo ni rafiki kwa shughuli zao za kila siku.

“Ajenda hii imepokelewa na kuna maelekezo kutoka juu, zoezi lenyewe bado halijasitishwa na hili zoezi la kuwaondoa machinga limeongelewa sana na watu wametafsiri wanavyofahamu,” amesema Mongella.

Wanga ambaye ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela amesema kuwa, pamoja na hoja hiyo kupokelewa na tayari kuna maelekezo yake kutoka juu (kwa rais) lakini linapaswa kuzungumziwa ili kuweka kumbukumbu.

“Sio kwa leo tu, hata 2020 itatusaidia kwenye kumbukumbu na hata kama tayari limekwisha tolewa ufafanuzi lakini katika suala la kumbukumbu ni mhimu na itatusaidia pa kuanzia,” amesema Wanga.

Kikao hicho kimewahusisha wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa manispaa, wabunge wa mkoa huo, wahandisi, kamati ya ulinzi na usalama mkoa na Meya wa Jiji hilo, James Bwire aliewakilishwa na Naibu Meya wake, Bhiku Kotecha.

error: Content is protected !!