MKUU wa mkoa wa Geita, Martin Shigella amesema amekubaliana na wakuu wa wilaya za mkoa huo kwamba hakuna mtumishi yeyote atakayekamatwa na kuwekwa ndani kwa sababu za kinidhamu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Geita … (endelea).
Pia amesema tangu ahamishiwe kushika wadhifa huo katika mkoa wa Geita, hajapokea malalamiko yoyote kutoka kwa wananchi, watumishi au viongozi kuhusu utendaji wa wakurugenzi au Baraza la Madiwani wa halmashauri za mkoa huo.
Shigella ametoa kauli hiyo leo tarehe 4 Machi 2023 katika mdahalo wa kujadili miaka miwili ya Serikali ya awamu ya sita madarakani chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema mtumishi anaweza kukamatwa na kufikishwa polisi iwapo atakuwa ametenda kosa la jinai lakini si katika masuala ya nidhamu.
Ametoa mfano kwamba mwalimu anaweza kuchelewa kikao kilichoitishwa na mkuu wa wilaya kwa sababu mwanaye ameumwa ghafla hivyo jambo kama hilo halipaswi kuchukuliwa kimabavu na mkuu wa wilaya kwa kumuweka mwalimu huyo ndani kisha kachelewa kikao.
“Kumuweka mwalimu mahabusu saa 48 kwa sababu ya kuchelewa kikao ni jambo la kishamba, hili halina nafasi kwenye mkoa wetu.
“Hayo ndio maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, alituelekeza sisi wakuu wa mikoa. Niwahakikishie hutasikia hilo jambo kwa sababu tuna kazi kubwa ya kufanya si kuja kugombana.
“Niwahakikishie hutasikia hilo jambo kwa sababu tuna kazi kubwa ya kufanya si kuja kugombana hizi nafasi ni dhamana tu,” amesema.
Aidha, amesema ana miezi sita ya uongozi kwenye mkoa, lakini hajapata malalamiko kuwahusu wakurugenzi au viiongozi wengine wa mkoa huo.
Leave a comment