December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

RC Dar: Mgawo wa maji utaendelea

Spread the love

 

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Amos Makalla amesema mgawo wa maji jijini humo utaendelea kuwepo mpaka pale mvua zitakapoanza kunyesha na kuongeza kina cha maji kwenye vyanzo vya maji Ruvu Chini na Ruvu Juu ambavyo kwa sasa vina upungufu wa maji. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

RC Makalla amesema hayo juzi Jumanne, tarehe 23 Novemba 2021, wakati wa ziara ya kutembelea vyanzo vya maji vya Ruvu Juu na Ruvu Chini akiambatana na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa na watendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) iliyolenga kujionea na kujiridhisha hali ya maji kwenye vyanzo hivyo.

Akizungumza katika ziara hiyo, Makalla alisema baada ya maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa yamesaidia uwepo wa ongezeko la lita milioni 200 kutoka lita milioni 65 na kufanya upungufu wa lita milioni 70 kwa Ruvu Chini.

Aidha, Makalla alisema upande wa Ruvu Juu Hali sio mbaya sana kutokana na uzalishaji wa maji kuendelea kuwa lita Milioni 196 kwa siku.

Kutoka na hilo, Makalla alitoa wito kwa wananchi kutumia maji vizuri na kuendelea kutunza vyanzo vya maji huku akipongeza jitiada zinazofanywa na wizara ya maji na DAWASA.

Hata hivyo, Makalla alisema mahitaji ya maji kwa mkoa wa Dar es Salaam kwa siku ni Lita Milioni 540 na uzalishaji Lita Milioni 520 na asilimia kubwa ya Maji hayo yanategemea kunyesha kwa mvua lakini Kukosekana kwa mvua za Vuli kwa takribani miezi miwili Sasa imesababisha upungufu wa maji.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA, Mhandisi Cyprian Luhemeja alisema mamlaka hiyo inaendelea kufanya kila jitiada kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya maji licha ya kuwepo kwa mgawo.

Kwa mujibu wa DAWASA, mtambo wa maji Ruvu Juu unazalisha lita milioni 196 kwa siku na mtambo wa Maji Ruvu Chini unazalisha lita milioni 270 kwa siku lakini kutokana na upungufu wa maji kwa sasa unazalisha lita milioni 200 pekee na kufanya uwepo wa mgao wa maji.

error: Content is protected !!