January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

RC Dar asimulia A-Z tukio la moto Kariakoo “yangetokea maafa makubwa”

Spread the love

 

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC) nchini Tanzania, Amos Makalla, amesema kama juhudi za kuudhibiti moto katika Soko Kuu la Kariakoo, zingechelewa kufanyika, kungetokea maafa makubwa zaidi ya yaliyotokea. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Makalla ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, tarehe 12 Julai 2021, mbele ya Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene, alipotembelea soko hilo kwa ajili ya kuona shughuli za uzimaji moto zinazoendelea kufanywa na Jeshi la Zima Moto na Uokoaji nchini.

Moto huo ulizuka usiku wa Jumamosi, tarehe 10 Julai 2021, hadi sasa chanzo chake hakijulikani, lakini Serikali imeunda tume ya uchunguzi wa tukio hilo, inayotarajiwa kutoa ripoti yake Jumapili, tarehe 18 Julai 2021.

“Mimi nilikuwepo tangu siku ya tukio, nimekesha na nimelala hapa na wala sijasimuliwa.”

“Kazi yote iliyofanyika hapa nimeona. Changamoto walizotaja ni kweli namna magari kuingia na kutoka ilikuwa shida, wamefanya kazi kubwa bila ya hivyo ingekuwa maafa makubwa zaidi,” amesema Makalla.

Akisimulia tukio hilo, amesema awali jeshi hilo lilifanikiwa kuudhibiti moto huo, lakini bahati mbaya upepo ulivuma na kuongeza kasi ya uwakaji moto huo, na kusababisha maji katika magari ya zimamoto kuisha.

“Kazi imefanywa kubwa na vibanda 99 ambavyo wameweza kutoa mali. Hapa tulipokuja moto ulianza chini, ulielekea kuzimwa ila kule juu kukaanza kuwaka. Hapa kulikuwa na duka viuatilifu moto ulikuja kukawa kama kuna mlipuko, ulipotoka juu kurudi chini kwa ile hewa ukalipuka kwa kasi kubwa,” amesema Makalla.

Muonekano wa soko la Kariakoo baada ya kuungua moto

Mkuu huyo wa Mkoa, amesema awali waliruhusu baadhi ya wafanyabishara kuchukua mali zao, lakini moto ulipozidi wakawazuia ili kuepusha majanga zaidi.

“Na pale moto wakati tunaendelea kuudhibiti watu wakaja kuchukua mali zao, tulipoona moto umezidi, tukaona itatokea maafa mengine kama tutaendelea ruhusu watu kuchukua. Tukazuia,” amesema Makalla.

Hata hivyo, Makalla amesema, Jeshi la Zima Moto na Uokoaji lilifanikiwa kudhibiti moto huo usisambae maeneo mengine ya soko na katika maduka ya jirani.

“Kudhibiti moto kulipotushinda, tukaona tuangalie namna ya kudhibiti usiende nyumba za jirani, soko dogo na la chini. Moto ulipanda juu ikawa shida huwezi ona tukawa tunamwaga maji kwenda juu. Kazi iliyokuwepo ni kuendelea kudhibtii usitoke nje,” amesema Makalla.

Makalla amesema , Jeshi la Zima Moto lilifanya kazi kwa shida kwa kuwa lililazimika kufuata maji mbali na eneo hilo, kutokana na mabomba yaliyokiwepo jirani kutokuwa na presha kubwa ya kutoa maji.

Amesema lilikuwa linachukua maji kutoka maeneo ya Bandari ya Dar es Salaam na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, mkoani humo.

“Jeshi limefanya kazi kubwa pamoja na changamoto zilizojitokeza maji kufuata huko, lakini haikukwamisha magari yaliendelea kupishana ya bandari na airport,” amesema Makalla.

Akielezea athari za tukio hilo, Makalla amesema umeathiri biashara za watu zaidi ya 200, huku 99 wakifanikifanikiwa kuokoa mali zao. Na 397 wenye vizimba vya biashara katika soko la chini wakinusurika katika mkasa huo.

“Soko lile la chini kuna wafanyabishara 397, hawatakuwa wamethirika na vibanda 99 wamiliki wake walifanikiwa kutoa mali zao. Walioathirika ni wale 224,” amesema Makalla.

Makalla amesema kwa sasa wafanyabiashara hawaruhusiwi kuingia eneo la tukio, hadi pale Kamati ya Ulinzi na Usalama itakapojiridhisha kama moto huo umezimika kabisa.

error: Content is protected !!