June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

RC awaonya madiwani Msalala

Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda

Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda

Spread the love

MKUU wa mkoa wa Shinyanga, Ally Rufunga amewataka madiwani wa Halmashauri ya Msalala kuheshimu maamuzi yaliyotolewa na ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu ujenzi wa makao makuu ya halmashauri hiyo, vinginevyo serikali itaifuta mara moja iwapo wataendelea na malumbano. Anaandika Mwandishi wetu, Shinyanga … (endelea).

Rufunga ametoa tamko hilo juzi alipokuwa akitoa taarifa ya majibu ya ofisi ya waziri mkuu katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) ambapo alisema waziri mkuu ameagiza kuheshimiwa kwa maamuzi yaliyotolewa hapo awali ya makao makuu hayo kujengwa katika kata ya Busangi na si vinginevyo.

Amesema kwa kipindi kirefu baadhi ya madiwani wamekuwa wakishinikiza kubadilishwa kwa maamuzi yaliyotolewa hapo awali ambapo walikubaliana kwa pamoja kupitia kuwa makao makuu ya halmashauri hiyo yajengwe Busangi.

Hata hivyo, katika hali isiyokuwa ya kawaida baadhi ya madiwani walishinikiza kubadilishwa kwa maamuzi hayo hali iliyosababisha pia wajumbe wa kamati ya ushauri ya mkoa kushawishika na kumuagiza mkuu wa mkoa amwandikie barua waziri mkuu ili amuombe Rais Jakaya Kikwete aridhie makao makuu sasa yajengwe kata ya Segese.

Kutokana na hali hiyo, mkuu wa mkoa alimwandikia barua waziri mkuu yenye Kumb. Na. CAB.263/290/02B/39 ya Machi 20, 2014, akimuomba amshauri Rais Kikwete aridhie maoni ya madiwani waliomba kufanyike mabadiliko ya ujenzi wa makao makuu yajengwe kata ya Segese badala ya Busangi.

Hata hivyo, mapendekezo hayo yalikataliwa kwa barua ya ofisi ya waziri mkuu yenye Kumb. Na. PM/P/1/567/74 ya 26 Juni 2014, iliyoagiza kuheshimiwa kwa maamuzi ya awali yaliyotolewa na vikao halali juu ya ujenzi wa makao makuu ya halmashauri hiyo na ibaki kuwa katika kata ya Busangi kama ilivyokwisha amriwa.

“Naomba niwape taarifa juu ya maelekezo yaliyotolewa na ofisi ya waziri mkuu kuhusu suala hili, tumeagizwa tuheshimu maamuzi yetu ya awali, ujenzi wa makao makuu ya halmashauri ya Msalala uendelee kubaki kata ya Busangi na si vinginevyo.

 “Na niwaeleze wazi Serikali sasa imechoka kusikia malumbano haya yaliyosababisha kuchelewesha maendeleo ya wananchi huku fedha zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi huo zikikaa bila ya kufanya kazi, badala yake sisi tunaendelea na malumbano yasiyo na maana wala tija kwa wananchi wetu,” alieleza Rufunga.

Amefafanua kuwa yapo mambo matatu yanayoweza kujitokeza hivi sasa katika suala hilo, kwamba mojawapo ni kukubali makao makuu yabaki pale pale kata ya Busangi, la pili kuteua eneo lingine mbali ya kata za Segese na Busangi na mwisho iwapo itashindikana kabisa basi ni kuifuta halmashauri hiyo.

Amesema “kutokana na baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo ya Msalala kukaidi agizo hilo la waziri mkuu, basi ni vizuri wakae wasubiri maamuzi ya mwisho yatakayotolewa na serikali kuu ambayo huenda yasiwe mazuri kwao.”

Kwa takribani miaka miwili sasa madiwani wa Msalala wamekuwa wakivutana pasipo mafanikio juu ya ujenzi wa makao makuu ya halmashauri hiyo ambapo baadhi wamekuwa wakisisitiza kuheshimiwa kwa maamuzi yaliyotolewa awali na wengine wakitaka yajengwe kata ya Busangi.

error: Content is protected !!