August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

RC Arusha ataka ushahidi ‘majina feki’ waliokubali kuhama Ngorongoro

Spread the love

 

MKUU wa Mkoa wa Arusha, John Mongella amewataka watu wanaodai kuna majina ya kughushi katika orodha ya wananchi waliokubali kuhama kwenye Hifadhi ya Ngorongoro, walete ushahidi ili kuisaidia Serikali kujua ukweli. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mongella ametoa wito huo leo Jumanne, tarehe 15 Machi 2022, akizungumza kwa simu na MwanaHALISI Online, alipoulizwa ufafanuzi wake kuhusu madai yaliyotolewa na viongozi wa Kimila ‘Malaigwanani’ wa Wilaya ya Ngorongoro, kuwa hawakushirikishwa katika mchakato huo.

“Ikitokea mtu akasema huyu siyo wa Ngorongoro atakuwa amethibitisha mimi siwezi kukubali au kukataa. Kama wanaona kwenye orodha huyu sio wakasema ingekuwa msaada kwetu sababu zoezi ni shirikishi wao wenyewe wasimamie hilo zoezi,” amesema Mongella.

Aidha, Mongella amesema kuna timu maalumu iliyoundwa kwa ajili ya kusajili watu hao, na kwamba majina yao huthibitishwa kama ni kweli wanaishi hifadhini humo.

Akizungumzia madai ya kukaidi agizo la Rais Samia la kukutana na Malaigwanani wa Ngorongoro, Mongella amesema “kwanza waulize vizuri kama kweli tokea Rais aagize kama sijakutana nao. Mimi nilikutana nao mwaka jana Loliondo tukaongea.”

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella

Kuhusu kutoalikwa kuzungumza na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Mongella amesema jukumu hilo halikuwa la ofisi yake, kwani malaigwanani wana utaratibu wa kualikana wenyewe.

“Kuhusu wao hawakualikwa, utaratibu wa vikao vyao unajulikana, wenyewe wanaalikana sio sisi tunawaalika. Kusema walialikwa au hawakulaikwa, sisi sio waalikaje wa vikao vyao hivyo inakuwa ngumu kuthibitisha labda waseme wenyewe,” amesema Mongella.

Mongella amesema zoezi la kuwahamisha wananchi wanaoishi Ngorongoro ni la hiari na kwamba Serikali inaliendesha kwa mujibu wa sheria na misingi ya utawala bora.

Wakati huo huo, Mongela amewaomba wananchi kuweka maslahi ya Taifa mbele katika kushughulikia suala hilo.

“Mimi nafikiri watu watizame maslahi mapana ya Taifa letu, hii nchi ni yetu sote si ya kundi fulani. Tutizame maslahi ya nchi ili vizazi vyetu vidumu. Kwa hivyo waamue kwa maslahi ya nchi,” amesema Mongella.

“Ukienda pale Geita Gold Mine, kulikuwa na vijiji kadhaa, ukienda Nyamongo mkoani Mara, kule kuna migodi, kulikuwa na vijiji, ukienda Kusini mkoa wa Lindi kuna mitambo ya kuchakata gesi, kulikuwa na makazi ya watu, kila sehemu watu wanapisha,”

“Uzuri sheria zetu zinasema kama kuna maslahi sheria itekelezwe watu watolewe kwa fidia stahiki, watolewe kwa mazingira ya kibinadamu na sisi ndicho tunachokisema, hapa ni maslahi mapana ya nchi hakuna mtu anamchukia au kumnyanyasa mtu.”

Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Malaigwanani Wilaya ya Ngorongoro, Metui Ole Shaduo, alisema wananchi wa hifadhi hiyo hawako tayari kuondoka kwa kuwa walihamishwa zaidi ya mara moja, ambapo kabla ya 1959, walikuwa katika Hifadhi ya Serengeti.

Shaduo alidai, mgogoro huo unachochewa na kitendo cha malaigwanani wanatoka nje ya wilaya hiyo, kushirikishwa katika kutoa maamuzi huku wao wakiachwa.

error: Content is protected !!