June 22, 2021

Uhuru hauna Mipaka

RC ajikomba kwa JPM

Spread the love

WAKATI ‘mzuka’ wa Baraza la Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha) ukishuka baada ya kusitisha kusudio lao la ‘kuisaidia’ polisi kutekeleza agizo la Rais John Magufuli pia Jeshi la Polisi nchini, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma naye amejitosa, anaandika Dany Tibason.

Jordan Rugimbana, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma amekuja na tamko lake leo kwamba, mtu au kikundi ambacho kinadhani kufanya fujo katika mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ‘atakula naye sahani moja’ kwani Dodoma si salama kwa watu wenye nia ovu.

Rugimbana anatoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache tu baada ya viongozi wa Bavicha kutangaza vijana wake kutulia amri ambayo iliyoka kwa Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa.

Kumekuwepo na vuta nikuvute kwa takribani wiki tatu kati ya Jeshi la Polisi na Bavicha pia Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kuhusu kuzuia mkutano huo kwa mujibu wa maelezo ya polisi kwamba, hali nchini hairidhishi.

Wakati muafaka ukiwa tayari umepatikana kabla ya mkutano mkuu maalumu wa CCM kuelekea kumkabidhi madaraka ya uenyekiti wa CCM Dk. Magufuli kutoka kwa mwenyekiti wa sasa Dk. Jakaya Kikwete, Rugimbana amejitokeza na ‘kunogesha’ kuwa, Dodoma si mahala pa uovu.

Ametoa kauli hiyo leo alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya shughuli mbalimbali za kitaifa ambazo zinatarajiwa kufanyika mapema mjini humo.

Amesema, kutokana na kuwepo kwa matamshi mbalimbali ya baadhi ya vikundi kudai kuwa, vina malengo ya kuzuia mkutano wa CCM, ametaadhalisha  kuwa, kwa sasa Mkoa wa Dodoma “siyo salama kabisa kwa mtu au kikundi cha watu ambao wanadhani wanaweza kuonesha umaarufu wao au kufanya fujo katika mkutano huo.”

Rugimbana ambaye kwa Mkoa wa Dodoma ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama amesema, kamwe katika kipindi hiki na kipindi chochote kile Dodoma haitaweza kuruhusu watu kuchezea amani iliyopo.

Licha ya kutokutaja majina na vikundi hivyo wala mtu yoyote lakini inaonesha wazi kuwa, kauli ya Rugimbana inailenga Bavicha ambao awali walitangaza msimamo wao wa kutaka kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa lengo la kuzuia mikutano yote ya kisiasa ili kutimiza lengo la Rais Magufuli.

“Nawatangazia Watanzania wote hasa wale ambao wana nia ya kufanya fujo au kikundi cha watu ambao wana nia ya kufanya fujo katika mkutano mkuu wa CCM, wasijaribu kabisa hata kama wapo ambao wameonekana kukiri na kufuta nia yao ya kutaka kufanya zuio katika mkutano wa CCM lakini hatuwezi kufumbia macho.

“Kwa Mkoa wa Dodoma ulinzi upo wa kutosha na anayedhani kuwa anaweza kufanya fujo, kuonesha umaarufu wakae wakijua kabisa kuwa Dodoma ya leo siyo salama kwao,” amesema Rugimbana.

Wakati huo amesema, katika Mkoa wa Dodoma kwa sasa kuna matukio makubwa ambayo yanaufanya mkoa kuwa na viashiria vya kuwa Makao Makuu.

Ametaja shughuli hizo kuwa ni kesho saa 10 jioni Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu anatarajiwa kuzindua ujenzi wa uwanja wa ndege kwa awamu ya kwanza kwa niaba ya Rais Magufuli.

Amesema, upanuzi huo wa uwanja wa ndege unaozinduliwa na Waziri Mkuu ni kwa ajili ya kuwezesha usafiri wa anga kuwa mwepesi na kuufanya Mkoa wa Dodoma kuwa na wepesi wa kufikiwa.

“Tumekuwa na mtandao wa barabara,lakini hatukuwa na uwanja wa ndege wa kupokea ndege kubwa lakini kwa sasa tutakuwa na uwezo wa kutumia ndege na kwa njia hiyo fursa kubwa ya wafanyabiashara na watu wengine kutumia uwanja wa ndege” amesema Rugimbana.

Kwa hatua nyingine amesema, maandalizi ya ujenzi wa Viwanja vya Mashujaa pamoja na kujenga mnara kwa maana ya kusherekea sikukuu ya mashujaa, yanaendelea vizuri na kuwa, kwa mara ya kwanza yatafanyika mjini Dodoma ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais Magufuli.

Amesema, katika maandalizi hayo ya mashujaa, mashujaa wameisha fika katika viwanja hivyo kwa ajili ya kufanya mazoezi.

Kutokana na ugeni mkubwa ambao hupo mkoani hapa Rugimbana amewataka watoa huduma mbalimbali kuhakikisha wanatoa huduma bora ambazo zitakuwa zikiwaridhisha watumiaji.

HALI YA DODOMA

Matamko mbalimbali ambayo yanatolewa na Bavicha yameonesha wazi kuwatia kiwewe viongozi wa CCM na kulazimika kuwa na ulinzi mkali.

Katika hali isiyokuwa kawaida, ulinzi umeimarishwa zaidi tofauti na mikutano mikuu yote ya CCM kutokana na jengo la CCM Makao Makuu kuzungukwa na walinzi ambao ni vijana wa CCM.

Kwa kawaida jengo la CCM Makao Makuu lima milango mitatu ambao mlango mmoja mkubwa ni kwa ajili ya kupitisha magari, mlango mdogo upitiwa na watu kwa njia ya kawaida hususani waandishi wa habari na mlango mwingine hutumiwa na watu wote.

Hata hivyo, kwa siku ya leo imekuwa tofauti kwani kila kona kuna ulinzi huku UVCCM wakiwa wanafanya ulinzi kwa kuzuia njia ambazo zinatakiwa kupitiwa.

 

error: Content is protected !!