January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Raundi ya 8 Ligi Kuu Bara, Simba yazama, Azam, Yanga nguvu sawa

Spread the love

BAADA ya kusimama kwa mwezi mmoja na nusu, hatimaye Ligi Kuu Tanzania Bara imerudi tena katika raundi ya nane iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita.

Katika hatua hiyo jumla ya michezo saba imechezwa huku michezo iliyovuta hisia za mashabiki wa soka Tanzania ni kati ya Simba na Kagera, Yanga na Azam na ule wa Mtibwa Sugar na Stand United ambao ulichezwa kwa siku mbili.

Simba ambao walikuwa nyumbani walijikuta wameangukia pua baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0, shukrani kwa Atupele Green akitumia vizuri makosa ya kipa Ivo Mapunda.

Kwa matokeo hayo Simba imebaki na pointi tisa ikiwa nafasi ya kumi baada ya kucheza michezo hiyo nane.

Mchezo mwingine uliochezwa kati ya Yanga na Azam FC ambao ulimalizika kwa sare ya 2-2. Mabao ya Yanga yamefungwa na Amisi Tambwe na Simon Msuva, wakati ya Azam FC yamefungwa na Didier Kavumbangu na John Bocco.

Vinara wa ligi hiyo, Mtibwa Sugar imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Stand United katika mwendelezo wa mchezo uliochezwa kwa siku mbili baada ya siku ya kwanza kuhairishwa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.

Mtibwa inabaki kileleni mwa Ligi Kuu kwa kufikisha pointi 16 baada ya mechi nane, ikifuatiwa na Azam FC na Yanga zenye pointi 14 kila moja.

Mbeya City imeibuka na ushindi wa 1-0 katika mchezo wa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara. Bao la Mbeya City limefungwa na kiungo mshambuliaji, Deus Kaseke. MCC inatimiza pointi nane baada ya mechi nane, hivyo kujivuta hadi nafasi ya 11 kutoka mkiani. Ndanda inayobaki na pointi zake sita, sasa ndiyo inashika mkia.

Polisi Moro imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mgambo JKT, mabao yake yakifungwa na Nicholas Kabipe na Imani Mapunda.

Ruvu Shooting wao waliibuka na ushindi wa bao moja dhidi ya ndugu zao JKT Ruvu mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam. Bao la Ruvu limefungwa na Hamisi Suleiman.

Katika mechi nyingine Coastal Union imelazimisha sare ya bila kufungana na wenyeji Prisons Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya. Matokeo hayo, yanaifanya Coastal itimize pointi 12 baada ya kucheza mechi nane, wakati Prisons nayo inatimiza pointi saba baada ya mechi nane pia.

Ligi hiyo itaendelea tena Januari 3 mwakani kwa mechi tano, Coastal Union itacheza na JKT Ruvu katika Uwanja wa Mkwakwani, Ruvu Shooting itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mabatini, Azam itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Azam Complex, Stand United itakuwa mgeni wa Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri wakati Mbeya City na Yanga zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa Sokoine.

Ligi hiyo ambayo itachezwa mfululizo (non-stop) hadi itakapomalizika Mei 9 mwakani, itakamilisha raundi ya tisa Januari 4 mwakani kwa mechi kati ya Mgambo Shooting na Simba kwenye Uwanja wa Mkwakwani, na Tanzania Prisons itakayokuwa mwenyeji wa Ndanda kwenye Uwanja wa Sokoine.

error: Content is protected !!