June 19, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais wa Colombia atwaa tuzo ya Nobel

Spread the love

JUAN Manuel Santos, rais wa Colombia ameshinda Tuzo ya Amani ya Nobel kwa mwaka 2016 baada ya kufanikiwa kuingia makubaliano ya amani na waasi wa Farc nchini humo na kusitisha vita vilivyodumu kwa karibu miaka hamsini, anaandika Charles William.

Wakati Rais Santos akishinda tuzo hiyo kufuatia mkataba wa amani wa kihistoria Colombia, tayari mkataba huo wa kusitisha vita na waasi umeshavunjika.

Rais Santos aliingia mkataba wa amani na kiongozi wa waasi hao Rodrigo Londono ‘Timochenko’ mjini Cartagena tarehe 27 Septemba, mwaka huu na alinukuliwa akisema, “Colombia inasherehekea, ulimwengu unasherehekea, kwa sasa kuna vita vimemalizika duniani.”

Ingawa mkataba huo ulikutana na ukosoaji mkubwa, wakosoaji wadai kuwa mkataba huo wa amani unawanufaisha waasi wa Farc na kuwapa fursa ya kukwepa kuwajibishwa na vyombo vya sheria kutokana na makosa ya uhakifu wa kivita waliyofanya.

Hata hivyo Rais Santos alinukuliwa akisema kuwa hayo ndiyo mapatano bora zaidi yanayoweza kufanywa kwa niaba ya Colombia.

Watu zaidi ya 260,000 waliuawa, kwenye vita hivyo na wengine milioni sita kuachwa bila makazi kutokana na uharibifu wa miundombinu na makazi.

Siku tano tu tangu kuingiwa kwa makubaliano hayo ya amani katika taifa hilo na kulifanya kundi la waasi la Farc kuweka silaha chini, wananchi walipiga kura ya ya maoni na kuyakataa mnamo Oktoba 2.

Baadhi ya wanachama wa Farc, pamoja na maafisa wa kijeshi na polisi walipangiwa kufikishwa mbele ya mahakama maalumu kujibu mashtaka kwa makosa ambayo wametekeleza katika vita nchini humo chini ya mkataba huo.

Kundi la Farc, ambalo lilianza kama wanamgambo wa Chama cha Kikomunisti mwaka 1964, linatarajiwa kuacha vita na kuingia katika siasa za amani.

error: Content is protected !!