Thursday , 28 March 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Rais usiwaendekeze kijani wakupingao ndani
Makala & Uchambuzi

Rais usiwaendekeze kijani wakupingao ndani

Aliyekuwa Spika wa Bunge, Job Ndugai
Spread the love

 

JAPO mimi siyo mwanachama wa chama chochote cha siasa nchini, hata hivyo, bado nitavitazama vyama vyote kwa jicho sawa hasa ikizingatiwa kuwa ndivyo wenye dhamana ya kuongoza Taifa letu pale chochote kinapopewa ridhaa na Watanzania. Anaandika Nkwazi Mhango … (endelea).

Leo nawasiliana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa mara ya kwanza. Sijawahi kuwa na ushabiki wa kuviandikia vyama au vikundi vya watu. Lakini nikiangalia namna mambo yalivyo nchini najikuta nikikiandikia chama tawala.

Kwanza, CCM ni chama tawala ambacho, kwa njia moja au nyingine, kinanihusu kama Mtanzania yeyote. Kwani, uwepo madarakani unagusa maslahi mapana ya Taifa ukiachia ya chama. Hivyo, CCM si chama tu bali chama tawala kilichopewa madaraka na Watanzania wengi kikaunda Serikali na kukamata dola kwa niaba yao.

Pili, nashangaa kunani watu wazima kuvuana nguo hadharani! Je ni kwa sababu gani na faida ya nani na kwanini? Je kuna bifu baina ya wakubwa wa chama au kuna kitu kimepungua ama kinakwenda ndivyo sivyo? Kwa wanaojua namna CCM inavyofanya mambo yao kwa mshikamano wa pamoja, inashangaza sana. Pia, hii ni hatari kwa chama ukiachia mbali aibu na hatari.

Tatu, naangalia hata kile kinachowagombanisha ambacho kiko wazi hasa mkirejea mipango na sera zenu kwa makini. Je, kama alivyosema Rais Samia Suluhu Hassan, hiki kinachowakuta ndiyo siasa za kuelekea mwaka 2025? Je, ili iweje na kwanini? Haraka ya nini? Je huu ndiyo utaratibu wenu?

Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan

Nne, najaribu kuangalia madhara yanayoweza kutokea kutokana na mnyukano wenu kama chama tawala hasa linapokuja suala la uendeshaji wa taifa letu hasa kiuchumi. Rais ambaye ndiye mkuu wa mhimili wa utawala na mwenye mamlaka makubwa kuliko wengine na Mwenyekiti wa CCM taifa hivi karibuni aliingia kwenye mtifuano na mkuu wa mhimili wa Bunge Job Ndugai aliyetahadharisha Watanzania na dunia kuwa nchi itapigwa mnada kutokana na kukopa.

Wakati Ndugai akipinga kukopa, Rais anasema Tanzania itakopa kwa vile haikopi kwenda kufuja bali kuwekeza kwenye maendeleo tena kwa mikopo isiyo na riba. Nani anapenda nchi yake iuzwe? Je Ndugai alipitiwa au kuna kitu nyuma ya pazia kuelekea 2025? Je Ndugai ni wa kupuuza, kuadhibu au kusikiliza? Je inawezekana Ndugui akasikilizwa na kueleweka akiwa ndani ya chama chake kwa kupingana na Serikali? Je hapa anangoja nini kufanya uamuzi mgumu japo kulinda heshima yake na kuonesha kuwa alimaanisha alichosema?

Tano, nikiangalia namna Ndugai alivyoomba kinachoitwa msamaha bila kukanusha madai yake ya kupinga kukopakopa hali ambayo itasababisha nchi kupigwa mnada kama alivyodai.

Nadhani kama chama kikongwe na tawala, fanyeni uamuzi mgumu tena haraka ili kulinda heshima ya chama. Hapa niseme kuwa msimchukulie Ndugai hatua peke yake bali na wengine wote wanaokinzana na mipango na sera zenu. Wafukuzeni uanachama baada ya kuwaita wajitetee na kusikiliza mashiko ya hoja na madai yao. Mfano, Ndugai kwa kukinzana na Mwenyekiti wa chama chake, amepoteza udhu wa kukiwakilisha chama kwenye mhimili husika kama kilivyoaminiwa na wapiga kura wa Tanzania.

Hivyo, ningekuwa mimi, ningeshapeleka barua kwa Katibu wa Bunge kuanzisha mchakato wa kumtafuta spika mwingine. Ndugai akifanya hivi, hatajisaidia yeye kubaki na heshima yake tu bali hata chama na mhimili wa Bunge. Hata huu mchezo unaoendelea wa kumshambulia Ndugai hauna afya wala tija kwa chama. Bila kufanya uamuzi mgumu, mtaendelea kushambuliana na kuvuana nguo hadharani kwa hasara na ni hatari yenu kwa baadaye. Lazima muonesha uongozi hapa.

Sita, suala la Ndugai ni fursa kwa CCM kuwashughulikia wote wanaopayukapayuka huku wakiendelea kuwa ndani ya chama au kuwa wabunge chini ya tiketi ya chama husika. Mfano, Josephat Gwajima (Kawe), Jerri Silaa (Ukonga) na Humphrey Polepole (Kuteuliwa) ambao wamekuwa wakionesha wazi kukinzana na mipango, misimamo na sera za chama hasa kuhusiana na namna ya kupambana na janga la Uviko-19.

Kama Watanzania wengine, wote wanaotajwa hapo juu, wana uhuru wa kutoa maoni yao, lakini hawana haki ya kupinga mipango, misimamo na sera za chama chao kinachoongoza nchi wakabaki na uhalali wa kuendelea kuwa ndani ya chama wanachokipinga. Wanapaswa wajiondoe au kuondolewa ili waendelee kuhubiri na kutetea kile wanachokiamini kama kweli wanakiamini na kina mashiko kwao na wengine.

Saba, najikumbusha historia ya matukio kama haya ndani ya CCM. Hebu jikumbushe kilichosababisha Waziri Mkuu mstaafu Mzee John Malecela kujiuzulu. Pale aliposhindwa kutetea sera ya CCM ya Muungano mbali na kumshauri vibaya Rais kuhusiana na kujiunga na Jumuia ya Nchi za Kiislam (OIC), aliambiwa arejeshe kadi au aachie ngazi na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na akaachia ngazi kulinda heshima yake na ya chama jambo wanalopaswa kufanya akina Polepole, Ndugai na Gwajima. Wakiendelea kutaka kula huku na kule, wafukuzeni uanachama na nyadhifa zao zitayeyuka zenyewe.

Ili kutoa onyo kwa wengine wanaotaka kula huku na kule, watimueni haraka sana ili wanaojiandaa kufanya kama hao wabunge nao washike adabu mbali na kujenga utamaduni wa watu kuwajibika kwa matamshi na misimamo yao na kile wanachoamini.

Hakuna awezaye kutumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja. Pia, nimshauri Mwenyekiti wa CCM, Samia akunjue makucha yake na kuparura ili wale wanaotaka kumhujumu washike adabu.

Kama alivyoahidi kufanya mabadiliko ya baraza la mawaziri ili kuwaweka huru wanaohangaika na uchaguzi wa mwaka 2025, awaruhusu pia wanachama wanaoanza kuhangaishwa na mnyukano huo wa 2025.

Kwani tukitafsiri maneno ya kimombo huwezi kuoka mkate wako na ukaula mwenyewe. Pia, mshika mbili lazima moja imponyoke atake asitake. Isitoshe, hawa ni watu wazima wenye akili na uamuzi wa kiutu uzima wanaopaswa kufanya uamuzi mgumu na wa kiutu uzima. Lakini kama watashindwa kufanya hivyo, si vibaya chama kikawasaidia kufanya uamuzi mapema hata kabla ya mwaka 2025.

1 Comment

  • Naomba muache uchafu na wizi huu wa kipuuzi. Inakuwaje mnatumia makala yangu hata bila kuandika jina langu eti mwandishi maalumu. Najua hamna waandishi nguli pamoja na watu kama Kubenea kuitwa nguli wakati hana elimu yoyote ukiachia mbali kubebwa na akina Ngurumo na mzee Ndimara zama zile. Mbona sasa hivi hatuuoni huu unguli wake?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nani anasema kuna hasara ATCL?

Spread the loveRIPOTI za makusanyo na matumizi ya fedha katika Kampuni ya...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Miaka 28 watumishi UDSM yaliwa na nzige, madumadu

Spread the loveGEORGE Francis anasikitika; anatembea akiwa na mawazo mengi, hajui la...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Nimekumbuka Samia wa miaka 3 iliyopita

Spread the loveWAKATI naandaa makala ya safu hii wiki hii, nimejikuta nakumbuka...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Hakuna fedha za Rais

Spread the loveKUNA mambo machache mazuri ya kujifunza kutoka kwa Margaret Thatcher,...

error: Content is protected !!