May 21, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Trump alipanga njama za wizi wa kura 

Rais wa Marekani, Donald Trump

Spread the love

RAIS anayeondoka mamlakani nchini Marekani, baada ya kushindwa uchaguzi mwezi uliyopita, Donald Trump, amedukuliwa kuwa alipanga njama za wizi wa kura. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Taarifa zilizochapishwa na gazeti la Washington Post la nchini humo zinasema, Trump amesikika akitoa maelekezo, kwa afisa mkuu wa uchaguzi katika jimbo la Georgia, kutafuta kura za kumuwezesha kubadilishwa kwa matokeo.

“Nahitaji kupata kura takribani 11,780, ili niweze kuendelea kuwa rais,” amesikika Rais Trump akimueleza katibu wa chama cha Republican, katika jimbo la Georgia, Brad Raffensperger.

Katika mazungumzo hayo ya siri, Bwana Raffensperger anasikika akimjibu Rais Trump, kwamba matokeo ya uchaguzi ya Georgia yalikuwa sawa.

Kwa mujibu wa shirika la utangazaji la Uingereza (BBC), gazeti la Washington Post, limenukuu maneno ya Rais Trump akisema, “njia nyingine ni kumshawishi na kumshinikiza katibu wa jimbo la Georgia, ili aweze kubadilisha matokeo.”

Mpaka sasa, ofisi ya Rais (Ikulu), haijasema lolote kuhusiana na mazungumzo hayo yaliyovuja.

Katika uchaguzi huo, Joe Biden alimshinda Rais anayeondoka madarakani katika jimbo la Georgia pamoja na majimbo mengine muhimu na kumuwezesha kupata kura 306 za wajumbe dhidi ya Bwana Trump aliyepata kura 232.

Tangu uchaguzi uliofanywa tarehe 3 Novemba 2020, Bwana Trump amekuwa akidai kuwa kura ziliibwa bila kutoa ushahidi wowote unaothibitisha madai yake.

Majimbo yote 50 yamethibitisha matokeo ya uchaguzi huo baadhi ya vituo ikiwa ni baada ya kura kuhesabiwa tena au pia kwasababu ya kesi zilizowasilishwa mahakamani kupinga matokeo.

Hadi kufikia sasa, Marekani imetupilia mbali kesi 60 zilizokuwa zimewasilishwa kupinga ushindi wa Bwana Biden.

Brad Raffensperger

Aidha, Bunge linatarajiwa kuidhinisha rasmi matokeo ya uchaguzi huo 6 Januari mwaka huu. Rais mteule Biden kutokea chama cha Democrat, anatarajiwa kuapishwa kama rais wa Marekani 20 Januari.

Pia, wapiga kura huko Georgia wanatarajiwa kupiga tena kura Jumanne kuchagua maseneta wawili wa jimbo hilo na matokeo ya uchaguzi huo huenda yakaweka sawa jinsi nguvu ya uongozi itakavyokuwa katika Bunge la Seneti.

Ikiwa washindani wawili wa chama cha Democrat watashinda, kunamaanisha kwamba kutakuwa na idadi sawa ya wabunge wa vyama vya Republican na Democratic na makamu mteule wa chama cha Democratic Kamala Harris ndiye atakayekuwa na usemi katika kura ya kufanya maamuzi.

Bwana Biden wa chama cha Democrat tayari anadhibiti bunge la wawakilishi.

Nini kilichotokea katika simu ya Trump?

Katika kipande kilichotolewa na gazeti la Washington Post, Bwana Trump anasisitiza kuwa ameshinda uchaguzi katika jimbo la Georgia na kumuambia Raffensperger, “hakukuwa na ubaya wowote kusema kuwa mumehesabu kura tena.”

Bwana Raffensperger alijibu kwa kusema: “Changamoto uliyonayo mheshimiwa Rais, ni kwamba takwimu ulizonazo wewe ni za uwongo.”

Baadaye katika simu hiyo, Bwana Trump alisema, uvumi uliopo ni kuwa kura zilizopigwa kwa njia ya posta zimeharibiwa na mashine ya kupiga kura iliondolewa kutoka kaunti ya Fulton jimboni humo – dai ambalo wakili wa Bwana Raffensperger amesema sio sahihi.

Baadaye rais alimtishia afisa huyo na kumtajia njia anazoweza kuchukua kisheria.

Alisema, unajua walichofanya na husemi lolote. Huo ni uhalifu. Huwezi kuacha hilo litendeke ukiwa kimya. Hiyo ni hatari kubwa kwako wewe na kwa Ryan, wakili wako.”

Kisha akaitisha kura za ziada 11,780 – ambazo zitafanya awe na jumla ya kura 2,473,634 jimboni humo, moja zaidi ya kura alizopata Biden (2,473,633).

Alimtaka Raffensperger kuchunguza tena matokeo ya uchaguzi katika jimbo hilo.

“Unaweza kuyachunguza tena lakini yafuatilie na watu ambao wanataka kupata majibu, wala sio wasiotaka kupata ufumbuzi,” alisisitiza Rais Trump.

Lakini akiongea kwa kujiamini, Bwana Raffensperger alisema, “Bwana Rais, unao watu wako wanaowasilisha taarifa na tuna watu wetu wanaowasilisha taarifa vilevile na kisha baada ya hapo yanafikishwa mahakamaani ambayo itafanya uamuzi.”

Akaongeza, “lazima tutetee matokeo yetu na tunaamini kuwa takwimu zetu ziko sahihi.”

Hata hivyo, Bwana Raffensperger hakutoa maelezo yoyote kuhusu ulaghai unaodaiwa na rais. “Hana taarifa yoyote!” Rais aliandika.

Bwana Raffensperger akajibu: “Kwa heshima, Rais Trump: Unachosema sio kweli. Ukweli utajitokeza.”

Afisa wa juu wa Democrat, Adam Schiff amesema: Kwa mara nyingine tena. “Jaribio la Trump kuingilia demokrasia liko wazi. Kupitia sauti iliyorekodiwa.”

Mwanasiasa wa Republican mwenye msimamo wa kati, Adam Kinzinger ameandika ujumbe kwenye mtandao wa Twitter akisema: “Bila shaka hii inachukiza. Kila mbunge anayefikiria kupinga matokeo ya uchaguzi huu, hawezi kufanya hivyo kwa nia moja.”

Je matokeo ya uchaguzi yataidhinishwa lini?

Kuna mgawanyiko katika chama cha Republican baada ya maseneta 12 kusema kuwa hawatapiga kura kuidhinisha ushindi wa Bwana Biden katika kikao cha Bunge la seneti Januari 6.

Ted Cruz aliongoza maseneta 11 akiitisha kucheleweshwa kwa mchakato huo kwa siku 10 ili kuchunguza madai ya wizi wa kura.

Makamu Mike Pence – ambaye kama rais wa bunge la Seneti anatarajiwa kusimamia kikao hicho na kumtangaza Bwana Biden mshindi amesema anaunga mkono hatua hiyo.

Bwana Pence hakurejelea madai ya wizi wa kura lakini mkuu wa wafanyakazi alisema Bwana Pence atashirikisha wengine kile anachosema ni “wasiwasi wa mamilioni ya Wamarekani kuhusu wizi wa kura na udanganyifu.”

Seneta wa Missouri Josh Hawley pia amesema kuwa atapinga matokeo ya uchaguzi kwasababu ya madai ya ukosefu wa uadilifu.

Wakati huohuo, maseneta wanne akiwemo Mitt Romney wametia saini taarifa inayosema watapiga kura kuidhinisha ushindi wa Bwana Biden.

error: Content is protected !!