RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema Watanzania wengi hawayajui makucha ya wakoloni kwa kuwa walizaliwa baada ya uhuru wa Tanzania Bara tarehe 9 Desemba 1961, hivyo hawakushuhudia madhila ya ukoloni. Anaripoti Regina Mkonde, Dar ea Salaam … (endelea).
Kiongozi huyo ametoa kauli hiyo leo Jumatano, tarehe 8 Desemba 2021, akihutubia Taifa kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru, kesho Alhamisi.
Kilele cha maadhimisho hayo, yatafanyika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa viongozi mbalimbali akiwemo Rais Samia na mgeni wake, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya.
Rais Samia amesema, kati ya Watanzania milioni 59 waliopo leo, ni Watanzania 2,520, 559, sawa na asilimia 4.3, walizaliwa kabla ya ukoloni.
“Takwimu hizi zinatuambia jambo jingine muhimu nalo ni kuwa Watanzania wengi walioko leo si tu hawakuwepo wakati wa uhuru bali pia na hawayakuishi madhila ya ukoloni wala matokeo yake.”
“Hivyo kwa kukosa kwao uzoefu wa hali ya huko nyuma, tulipotokea uwawia vigumu kutambua sababu za kujitoa katika makucha ya ukoloni na kujua thamani ya uhuru wetu,” amesema.
“Hatua kubwa tuliyopiga na mafanikio tuliyoyapa na tunayo yafaidi leo. Ni kwa sababu hiyo basi nikaona umuhimu wa kuhutubia taifa ili tukumbushane mawili matatu juu ya siku hii adhimu,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amewaomba Watanzania waendelee kudumisha uhuru wao, pamoja na kulinda amani na utulivu wa nchi.
Tanzania Bara ilipata uhuru wake tarehe 9 Desemba 1961, kutoka kwa ukoloni wa Waingereza, ambapo uhuru huo ulipatikana kutokana na harakati za Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na wenzake 16, akiwemo Abdul Sykes, Ally Sykes, Joseph Kaserabantu, John Rupia, Lameck Makaranga, Abdul Kandoro na Japhety Kiriro
Leave a comment