December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia: Wananiita ‘Bi Tozo’

Rais Samia Suluhu Hassan

Spread the love

 

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema kila anapozungumza kuhusu neno ‘tozo’ huwa linamgusa ndani ya moyo wake kwa sababu sasa mitandaoni wanamuita ‘Bi tozo’. Anaripoti Mwandishi Wetu… (endelea)

Rais Samia ametoa kauli hiyo kufuatia pendekezo la Baraza la Taifa la Usalama Barabarani kwamba nusu ya faini au tozo zinazotozwa na askari zielekezwe kwenye Baraza hilo ili lipate fedha za kujiendesha kwa kuwa halina bajeti yoyote inayotoka Serikalini.

Akizungumza katika maadhimisho ya Wiki nenda kwa usalama barabara yaliyofanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Kamanda wa Usalama barabarani Tanzania, SACP Wilbroad Mutafungwa pia aliomba baraza kuwezeshwa kupitia ruzuku ya bajeti ya serikali.

Maadhimisho hayo yalienda sambamba na kauli mbiu ya ‘Jali maisha yako na ya wengine barabarani.’

Aidha, akizungumzia mapendekezo hayo, Rais Samia amekataa pendekezo la faini au tozo zinazotozwa na askari trafki kutokana na makosa ya barabarani kugawiwa nusu kwa baraza hilo.

“Siungi mkono kwa sababu tozo tumeweka kama adhabu, sasa nguvu nyingi itatumika kutoza kwenye makosa kuliko kudhibiti makosa, Ni kweli tozo zitakuwa chanzo cha fedha kwenye baraza letu kwa kupata bajeti ya uhakika ya matumizi, lakini kuna njia nzuri zaidi.

“Ningependa kwa kiasi kikubwa tuende kudhibiti makosa ya barabarani tuepukane na tozo zinazolalamikiwa.

“Ninapozungumza tozo huwa linanigusa ndani ya moyo maana mitandaoni wananiita bi tozo, lakini bi tozo kwa njia nzuri ya kuleta maendeleo kwa Taifa letu. Na zitaendelea kuwepo zile za maendeleo kwa Taifa,” amesema

Aidha, ameeleza kusikitishwa na baraza hilo kufanya kazi mpaka sasa katika hali ya kutegemea misaada kutoka kwa wadau.

Amesema amebaini ukaguzi unaofanywa haufanyiki inavyopaswa, kwa sababu wakati mwingine mamlaka husika hutoa stika bila ukaguzi kufanywa.

“Nimeona bonge analala kwenye kile kidude  anachokonoa na zile spana zake, hii imeshapitwa na wakati… IGP tutumie vifaa vya kisasa katika ukaguzi ili tukague gari nyingi zaidi nchi nzima, tuuze stika nyingi na kukusanya fedha nyingi ambazo mapato yake yataelekezwa kwenye baraza hili,” amesema.

Aidha,  amesema kumekuwa na maombi mengi kutoka sekta binafsi kutaka kushirikiana na serikali katika kufanya kazi hiyo lakini maombi hayo yamekuwa yakiingizwa ndani na kutolewa nje miaka yote.

“Sasa naomba Jeshi la polisi, Wizara ya uchukuzi na ujenzi, Temesa kaeni mjadiliane jinsi mtakavyofanya kazi na sekta binafsi katika kufanya ukaguzi nchi nzima.

“Kwa sababu mkifanya na sekta binafsi mtafanya kwa uhakika, badala ya kuitwika  Serikali mzigo kununua mitambo, sekta binafsi itawekeza yenyewe.

“Mkishirikiana, mtafanya ukaguzi kwenye gari nyingi, stika zitauzwa, baraza litakuwa na fedha ya kujiendesha, pia mkifanya kazi na sekta binafsi mtaweza kuweka mifumo inayosomana na ambayo haitalalamikiwa. Badala ya kutaka kuajiri trafki wengi badilikeni muwe wa kisasa,” amesema.

error: Content is protected !!