SAMIA Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania, amewataka wananchi kudumisha amani na kuwaepuka walioanzisha “vichokochoko” kuwapuuza kwani hawawatakii mema. Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro … (endelea).
Rais Samia ametoa onyo hilo, jana Jumatano, tarehe 7 Julai 2021, alipokuwa akizungumza na wananchi wa Msamvu, mkoa wa Morogoro akisema, amani iliyopo nchini diyo msingi mkuu wa maendeleo ya taifa lolote duniani.
“Niwaombe sana ndugu zangu, vijichokochoko, vimeanza lakini naomba msivipokee, wanaokuja na vichokochoko wameshajua matumbo yao yanajaaje, chakula chao wanatoa wapi, pesa za matibabu watatoa wapi.”
“Nawaomba sana, wasije wakawaingiza mkenge. Kwa sababu pakichafuka ni wewe ndiyo utakaa ndani na mama watoto, msijue mtoto akiumwa utakwenda kumtibu na pesa gani,” alisema Rais Samia
Amri Jeshi Mkuu huyo alisema, “niwaombe sana tuendelee kuilinda amani na zinapotokea fujo, tunazijabili kwa haraka ili mambo yaendelee vizuri. Tuizunde amani yetu.”
Aidha, Rais Samia aliwataka wananchi wa eneo hilo na Watanzania kwa ujumla kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona kwa kufuata maelekezo ya wataalam wa afya ili kuepuka kupata maambuzi ya ugonjwa huo.
Rais Samia alisema baadhi ya maeneo nchini kama Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Dodoma tayari yana wagonjwa wa corona hivyo ni vyema wananchi wakafuata maelekezo ya wataalam.
Pia, aliwapongeza wakazi wa mkoa wa Morogoro kwa kuwa sehemu ya miradi mikubwa miwili ya kimkakati ya Reli ya Kisasa (SGR) na Mradi wa Kufua Umeme wa Mwalimu Nyerere katika mto Rufiji.
Alisema kutokana na kuwepo kwa miradi hiyo mkoani Morogoro ni vyema wananchi wakawa walinzi ili iweze kuwanufaisha wao na taifa kwa ujumla.
Aidha, Rais Samia amewahakikishia wakazi wa mkoa wa Morogoro kuwa changamoto mbalimbali zinazowakabili zikiwemo uhaba wa maji, migogoro ya ardhi, masuala ya afya na mengineyo kuwa serikali tayari imeshazifanyia kazi.
Leave a comment