October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia: Ukilikoroga nakutumbua bila kutazama kabila, Ma-RC miungu watu dawa yachemka

Spread the love

 

RAIS SAMIA Suluhu Hassan ameonya watumishi aliowateua kuacha kueneza sumu ya ukabila pindi wanapokosea na kutumbuliwa kwa sababu hateui kwa kuzingatia ukabila. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Pia amewaonya kwa mara ya pili wakuu wa mikoa kujiona miungu watu katika maeneo yao huku wateule wengine akitaka kujipusha na vitendo vya rushwa.

Rais Samia ametoa onyo hilo leo tarehe 11 Oktoba mwaka huu Ikulu Chamwino jijini Dodoma wakati akiwaapisha viongozi watatu aliowateua wiki iliyopita.

Viongozi walioapishwa ni Jaji Mustapha Siyani kuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Sophia Mjema kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na Jaji Omar Othmani Makungu, kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania.

Aidha, akizungumzia dhana ya ukabila, Rais Samia amesema hata katika mfumo wa makuzi shule na kwenye siasa, anamshukuru Mwalimu Nyerere kwani amewakuza Watanzania bila kuangalia makabila.

“Jambo lingine ninalotaka kusema kwa sauti kubwa, Samia Suluhu ninapotoka hakuna makabila kwetu kule Zanzibar tunajuana kwa maeneo, kuna waunguja Wapemba, Ukija Unguja kuna Watumbatu Wakunduchi, ukienda Pemba kuna Wakojani na wengine, kwa hiyo tunajuana hivyo,” Rais Samia – Dodoma.

“Kwa hiyo mimi binafsi niko hapa bila kuangalia kabila fulani, sasa watu wanafanya makosa, ukiwashika ukiwawajibisha, wanasema nimewajibishwa kwa sababu wa kabila fulani. Sina kabila”

Amesema hata ukimuuliza yeye ni kabila gani, atajibu kuwa ni Mzanzibar kwa sababu hana kabila.

“Kwa maana hiyo hata kwenye utendaji wangu wa kazi, sina kabila, uwe mmakonde, uwe mnani… ukikosea kwenye kazi mimi na wewe wala sitakufumbia jicho.

“Sasa kama ukitumbuliwa unalalamika ooh… mimi wa kabila fulani, hapana!. Hiyo sumu mnaipeleka sana, naomba isimame, Samia Suluhu mimi sina kabila Mwalimu Nyerere alitufundisha kufanya kazi bila kuangalia makabila ya watu. Sasa mkishikwa mnaasema kwa sababu wa kabila fulani,” amesema Rais Samia.

Rais Samia Suluhu Hassan

Amesema hata kwenye hotuba yake ya jana amesahau kuelezea ulinganifu wa takwimu za waliotumbuliwa katika kipindi cha miezi sita mwaka jana na mwaka huu.

“Lakini angalieni na ambao waliingia kwenye nanii wakafanya makosa nikawatoa, ni makabila mangapi, mimi siangalii kabila, naangalia unafanya kazi yako au hufanyi.

“Tamisemi kwa mfano kuna wa-tanga wangapi?, waziri M-tanga, Katibu Mkuu M-tanga, sijui nani huko M-tanga, nikaletewa nikaambiwa mama umeweka wa-tanga watupu, nikasema waacheni wafanye kazi, wakikoroga nawatumbua,” amesema Rais Samia na kuongeza;

“Unaletewa ooh mama hapa hukupanga vizuri kuna huyu na huyu wanatoka eneo moja… sasa so what, wana sifa au hawana! waacheni wafanye kazi. Anayekosea nitamuondoa. Sipangi kwa makabila, napanga kwa uwezo na nanayehisi atafanya kazi, tuende tukasukume maendeleo kwa wananchi.”

Aidha, Rais Samia amewataka wateule wake hasa wakuu wa mikoa, wajiepushe na vitendo vya rushwa pamoja na kuacha kuwa miungu watu katika maeneo yao ya kazi.

“Sitegemei kuona mkuu wa mkoa anaingia kwenye vitendo vya rushwa, sitegemeai na wala sitastahimili kuona mkuu wa mkoa anaingia kwenye rushwa,” amesema Rais Samia.

Amesema “hili nalirudia leo, sitegemei kuona wakuu wa mikoa wanakuwa waungu watu huko mlipo, kazi zenu zina miongozo kanuni na kila kitu, ambazo mnatakiwa kuzijua vizuri na mzifuate vyema. Mko kule kutumikia watu sio watu wawatumikie nyie.”

Pia, Rais Samia amewaagiza wakuu wa mikoa na wakurugenzi wa halmashauri wakasimamie vizuri fedha zilizotolewa na Serikali katika mpango wa kampeni ya maendeleo kwa ustawi na mapambano ya Ugonjwa wa Covid -19 (UVIKO-19), Sh. 1.3 trilioni.

“Fedha zilizomiminwa jana niwaombe wakuu wa mikoa mkafanye kazi, mkasimamie lakini kuletwa fedha zile waziri wa TAMISEMI (Ummy Mwalimu ) na katibu mkuu kusifanye halmashauri ku-relax kwenye kukusanya mapato, huo ndio mtihani wa kukurugenzi,” amesema Rais Samia na kuongeza:

“Fedha zile zimeletwa kutupa msukumo, lakini haina maana kwamba tumepata sisi tuache. Najua mna uwezo mkubwa kukusanya mapato, changamoto ni nyingi tunazoziondoa hapa hazifiki hata nusu ya zinazotukabili. Naomba mkakusanye mapato shughuli za maendeleo zikaendelee kule kwa wnanachi.”

error: Content is protected !!