May 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia: Tuzike tofauti zetu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Saluhu akihutubia Taifa mara baada ya kuapishwa

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassani, amewataka Watanzania kuzika tofauti zao na kwamba, sasa ni wakati wa kujiamini kama Taifa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Pia, amewataka kuwa wamoja katika kipindi hiki cha majonzi ya kufiwa na aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli (61).

Rais Samia ametoa wito huo leo Ijumaa tarehe 19 Machi 2021, Ikulu jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kuapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma kuwa Rais wa Tanzania, kufuatia kifo cha Dk. Magufuli.

Dk. Magufuli alifariki dunia Jumatano tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena iliyoko Dar es Salaam, wakati akipatiwa matibabu ya maradhi ya mfumo wa umeme wa moyo.

Akilihutubia Taifa la Tanzania kwa mara ya kwanza akiwa rais, amesema huu ni wakati wa kufarijiana na kuoneshana upendo.

“Kabla sijahitimisha, niwaase kusimama pamoja na kushikama katika kipindi hiki cha maombolezo. Huu ni wakati wa kuzika tofauiti zetu na kuwa wamoja kama Taifa, ni wakati wa kurafarijiana kuoneshana upendo,” amehimiza Rais Samia.

Amesisitiza “ni wakati wa kufutana machozi na kufarijiana ili tuweke nguvu zetu pamoja kujenga Tanzania mpya ambayo Hayati Rais Magufuli aliitamani.”

Kiongozi huyo mpya wa Tanzania, amesema huu ni wakati wa Watanzania kutazama mbele kwa kujiamini bila ya mashaka.

“Huu si wakati wa kutazama mbele kwa mashaka bali ni wakati wa kutazama mbele kwa matumaini na kujiamini, sio wakati wa kuyatizama yaliyopita, bali wa kutazama yajao, sio wakati wa kunyoosheana vidole bali ni wakati wa kushikana mikono na kusonga mbele,” amesema Rais Samia.

Aidha, amevishukuru vyombo vya ulinzi na usalama nchini, viongozi wa serikali wakiongozwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kusimamia vyema Katiba ya nchi, kwenye mchakato wa kubadilisha madaraka.

“Nitumie fursa hii, kuwashukuru viongozi wetu wa mihimili yetu muhimu Bunge na Mahakama kwa mshikamano waliyoonesha kipindi hiki, nimshukuru Rais Mwinyi (Hussein Mwinyi) na mihimili yake yote ya Zanzibar kwa kuwa na mimi bega kwa bega katika kipindi hiki kigumu,” ameshukuru Rais Samia na kuongeza:

“Niwashukuru wenzangu katika serikali wakiongozwa na Waziri Mkuu kwa kusimamia kipindi hiki cha mpito, niwashukuru wakuu wa ulinzi na usalama kutekelza wajibu wao ipasavyo chini ya katiba yetu kwa kuhakikisha nchi yetu inaenda kuwa ya amani na utulivu.”

“Nishukuru CCM kwa ukomavu wake madhubuti ambayo ndio msingi wa kuwezesha mabadiliko haya kwa amani na utulivu, niwashukuru vyama vya upiznani kwa salamu zao za kunipa faraja na mshikamno walizonifikishia baada ya kutangaza msibahuu mzito,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amewahakikishia viongozi wastaafu, kwamba katika uongozi wake hakuna jambo litakaloharibika.

Marais wastaafu waliko hai ni Mzee Ali Hassan Mwinyi na Jakaya Kikwete.

“Marais waliostaafu na waliofuatiwa na mpendwa wetu (Hayati Rais Magufuli), niwahakikishie hakuna jambo litakaloharibika,” ameahidi Rais Samia.

error: Content is protected !!