Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Rais Samia: Tunawasuta kwa utekelezaji miradi ya JPM
Habari za Siasa

Rais Samia: Tunawasuta kwa utekelezaji miradi ya JPM

Spread the love

 

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema mafanikio ya utekelezaji wa miradi iliyoanzwa katika serikali ya awamu ya tano, yanawasuta watu wanaosema uongo kwamba Serikali awamu ya sita imeitelekeza miradi hiyo.

Pia amewaagiza mawaziri kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa kwa fedha za mapambano dhidi ya Uviko -19, inatekelezwa kikamilifu kwani mwezi Juni ndio mwisho wa matumizi wa fedha hizo za mkopo nafuu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Tabora … (endelea).

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo tarehe 17 Mei, 2022 mkoani Tabora wakati akizindua ya barabara ya Nyahua- Chaya iliyojengwa kwa kiwango cha lami.

Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 85.4, imejengwa kwa msaada wa fedha zilizotolewa na Mfuko wa Serikali ya Kuwait.

Rais Samia mbali na kutaja miradi mbalimbali ya miundombinu ya barabara na madaraja ambayo inaendelea kutekelezwa na Serikali anayoiongoza, pia amesema miradi mingine mipya inakuja.

“Wanaposema serikali ya awamu ya sita imeacha kutekeleza miradi iliyoanzwa nyuma, hapa tunawasuta… wanachosema ni uongo, miradi yote tuliyoianza nikiwa Makamu wa Rais wa Serikali ya awamu ya tano tutaendelea nayo.

“Faraja yangu ni kwamba miradi kadhaa imekamilika tunaendelea na ujenzi, mingi itakamilika tutaanza mingine mipya ikiwemo daraja lililoombwa hapa la mto Loya, waziri analichukua. Ndio kazi ambayo serikali inafanya,” amesema Rais Samia.

Amesema lengo la serikali ni kuhakikisha anajenga miundombinu ya barabara na madaraja ili kuiunganisha mikoa na wilaya zote.

“Kwa kufanya hivyo, nina hakika tutachochea uzalishaji na biashara na hatimaye kuboresha maisha ya wananchi wetu,” amesema.

Pia amewataka wananchi kuilinda na kuitunza miundombinu hiyo ili itumike kwa muda mrefu badala ya kuiba vifaa vya usalama barabarani, kuchimba mchanga na kutupa taka.

Aidha, amesema Wilaya ya Uyui imepata kiasi cha Sh bilioni 3.7 ambacho ni fedha za mapambano dhidi ya Uviko-19 zilizotumika kujenga madarasa na shule mbalimbali shikizi.

Amesema licha ya kwamba Juni mwaka huu ndio mwisho wa matumizi wa fedha hizo Sh trilioni 1.3 zilizotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) kwa Serikali ya Tanzania Oktoba mwaka jana, bado baadhi ya halmashauri zinazungusha kutoa zabuni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa mbalimbali.

Ameagiza mawaziri kusimama fedha hizo kuhakikisha zabuni zote zinatekelezwa kwa wakati badala ya uzungushaji unaoendelea kwa lengo la kutoa mwanya wa matumizi ya rushwa.

“Tusipovuka asilimia 90 hatutapata fedha nyingine, maana yake uwezo wetu wa matumizi ni mdogo mno, tutapunguziwa kiasi kingine kitakachokuja.

“Ninawaagiza mawaziri muende kusimamia matumizi ya fedha hizi ili zile ambazo zipo kwenye bomba zitemwe kwa wakati,” amesema.

Pamoja na mambo mengine amemshukuru Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba kwa kuungana naye katika uzinduzi huo mkoani Tabora.

Rais Samia ambaye yupo Tabora kwa ziara ya kikazi, amesema jana baada ya kukutana Ikulu jijini Dar es Salaam na Profesa Lipumba na kufanya naye mazungumzo, alimweleza anaelekea Tabora.

Amesema Lipumba ambaye ni mwenyeji wa Tabora alimweleza kuwa hana ratiba ya kuelekea Tabora lakini ameonesha uungwana kwa kusafiri usiku ili kushiriki uzinduzi huo.

Awali Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema ujenzi wa barabara hiyo, imegharimu kiasi cha Sh bilioni 123.95.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Dk. Mwakyembe : Zanzibar waliongoza kutaka Serikali 2 za muungano

Spread the love  MWANASIASA mkongwe nchini, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema mjadala wa...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia ataja mikakati ya kufikia trilioni 2 biashara Uturuki, Tz

Spread the loveWakati Tanzania na Uturuki zikidhamiria kuongeza kiwango cha biashara hadi...

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

error: Content is protected !!