Wednesday , 24 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Rais Samia: Tuko tayari kuzungumza kuenzi kazi aliyoacha Maalim Seif
Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia: Tuko tayari kuzungumza kuenzi kazi aliyoacha Maalim Seif

Spread the love

 

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema katika kuenzi na kutumia busara aliyoiacha Aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad yupo tayari kukaa vikao kuleta suluhu kama lilivyo jina lake pale kutakapotokea mgongano wa hoja. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Pia amemuelezea Hayati Maalim Seif kwamba alikuwa daraja la amani na mtu aliyependa maridhiano ya kisiasa badala na malumbano na vurugu kama walivyo baadhi ya wanasiasa.

Rais Samia amesema hayo leo tarehe 5 Novemba, 2021 wakati akihutubia kwenye ufunguzi wa mkutano wa kumbukumbu ya maisha ya Maalim Seif katika ukumbi wa hoteli ya Golden Tulip – Zanzibar.

Akizungumzia maisha ya mwanasiasa huyo mkongwe aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo kabla ya kufariki tarehe 17 Februari, 2021, Rais Samia amesema si kawaida kwa binadamu kukutana katika kuwakumbuka marehemu wao kwa uzito mkubwa tena mwaka mmoja baada ya mpendwa wao kuondoka, kama ilivyotokea kwa Maalim Seif.

Amesema haishangazi kukutana kumkumbuka Maalim Seif kwani hata katika uhai wake alikuwa makutano ya watu.

“Tuliyemfahamu kwa miaka mingi tumemjua kama mtu wa kukutanisha watu, alikuwa kiongozi wa watu, anaishi na watu na watu wakamshiba katika mioyo yao,” amesema Rais Samia.

Amesema Maalim Seif mbali na kushirikia maridhianiano ya mwaka 2000, 2010, katika  uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ndiye tena aliyeshiriki na kufanikisha maridhiano baada ya uchaguzi huo.

Amesema utayari wake wa kuangalia masilahi mapana ya Taifa ndivyo vilivyofanikisha vyama vya CCM na ACT Wazalendo kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na Maali Seif kuwa makamu wa kwanza wa Rais.

“Hapa alifanya kazi kubwa, na tushukuru shani ya Mungu ya kutuwekea Maalim Seif ukitizama hali ilivyokuwa mwaka huu na presha aliyokuwa akiipata kutoka kwa vyama vyake na wale waliokuwa hawaitakii mema Zanzibar, lakini bado alichambua chuya na mchele akasema nadhani njia ya kwenda ni hii ili tutoke salama.

“Ni kama alijua atatuacha, kaifanya kazi ile kwa umahiri mkubwa na baada ya kumaliza Mungu hakumpa umri kamchukua, Mungu amlipe mema kule alikokwenda. Hii aliyofanya ilikuwa sadaka kubwa kwa nchi yetu.

“Kama kuna jambo la kulishika kwa mikono yote, si la kufanyia mzaha ni hii kazi aliyotuachia maalimm seif, umoja na mshikamano wa watu wetu, kuendeleza visiwa vyetu.

“Busara ileile itumike, tunapopingana kwa hoja vikao vitamaliza, vikao vitaleta suluhu, tofauti na mvurugano hauleti suluhu na kina suluhu tuko hapa, tutakuwa tayari na kuzungumza, lakini nasisitiza kuenzi kazi aliyotuachia,” amesema.

Rais Hussein Ali Mwinyi, akimwapisha aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Raisa wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad

Amesema licha ya kwamba Maalim Seif alifanya kazi ya ualimu hata kuitwa maalim, umaalim wake ni wa kipekee kwani hakuwa tu mwalimu wa wanafunzi bali pia alikuwa ni mwalimu wa watu.

“Maalim Seif alikuwa na uthibiti wa msimamo wake na alikuwa na utayari wa maridhiano hata pale unapotokea msigano. Na amefanya kazi hii ndani ya chama chake na katika vyama vingine.

“Tunaomfahamu Maalim Seif hata wakati akiwa CCM, enzi za chama kimoja alipokuwa na jambo alisimama na kuongea, na msimamo huo huo aliuendeleza hata alipohama na kuanzisha Chama cha Wananchi (CUF), alituheshimu na tulimuheshimu, hata alipotupinga hakuwa mwenye kutukana bali alitupinga kwa hoja,” amesema.

Aidha, Rais Samia ameongeza kuwa Maalim Seif siku za mwisho za uhai wake alihubiri ujumbe wa maridhiano na umoja wa kitaifa kokote alipopita.

“Tutakumbuka alifunga safari yeye na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi kwenda kumuona Rais John Magufuli (Hayati ) ambapo alisema utulivu na amani ya nchi ndio jambo la muhimu.

“Maalim ingawa kuna wakati aliingiwa na kinyongo lakini alikuwa tayari kuzungumza kwa maslahi ya Taifa… alionyesha utayari wa kuzungumza. Ni mtindo mzuri kuenzi waasisi wetu walioleta mchango mkubwa kwa Taifa letu. Ni jambo zuri, na njia pekee ya kumuenzi Maalim Seif ni kuenzi umoja na mshikamano uliopo,” amesema.

Amesema kama kuna somo Maalim Seif aliloliachia kwa wanasiasa, ni kuwa tayari na kuwa na msimamo wa kutafuta maridhiano kwa wale ambao unakuwa na tofauti nao.

“Maalim Seif alikuwa na uthabiti wa msimamo wake na alikuwa na utayari wa maridhiano hata pale unapotokea msigano. Na amefanya kazi hii ndani ya chama chake na katika vyama vingine,” amesema.

Aidha, amesisitiza wazungumzaji katika kumbukizi hiyo, wazungumzie zaidi kwenye eneo la maridhiano na umoja wa kitaifa ambao ndio maudhui makuu ya mkutano huo.

“Pia ni jambo la faraja kuona mjumuiko wa watu mbalimbali wenye mawazo na itikadi tofauti wamekutana kukumbuka maisha na mchango wake.

“Mjadala utachapusha mashirikiano kumjenga na kumstawisha mama yetu Zanzibar na Tanzania, tutoe fikra zitakazosaidia kufanikisha malengo mahsusi kumuenzi Maalim Seif.

Ameongeza; “Taasisi ya Maalim Seif Foundation ni yetu sote na tutaichangia, mkikwama katika masuala yoyote ya uendeshaji mtuone tuone tunasaidia vipi,” amesema Rais Samia.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

Habari za Siasa

Serikali kuanzisha mradi wa Gridi ya maji ya Taifa

Spread the loveWaziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema katika mwaka wa fedha...

error: Content is protected !!