May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia: Tuishi kwa kuacha alama

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa katika msiba wa Mhandisi Patrick Mfugale

Spread the love

 

SAMIA Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania, amewataka wananchi kila mmoja kwenye nafasi yake, kuhakikisha anatumia muda alionao kufanya mambo yatakayoacha alama pindi akiondoka duniani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Rais Samia, amesema hayo leo Ijumaa, tarehe 2 Julai 2021, katika shughuli ya kuuaga mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mhandisi Patrick Mfugale (67), katika viwanja vya Karimee, Dar es Salaam.

Mhandisi Mfugale, alifariki dunia ghafla asubuhi ya tarehe 29 Juni 2021, jijini Dodoma alipokuwa akihudhulia kikao. Mwili wake, utazikwa Jumatatu ijayo ya tarehe 5 Julai 2021, Kijijini kwao, Ifunda mkoa wa Iringa.

Rais Samia amesema, Taifa limempoteza mhandisi mahili na aliyekuwa tayari kulitumikia taifa hili kwa upendo mkubwa.

“Wote hapa hakuna aliyechagua siku ya kuzaliwa au kuondoka hapa duniani, ni mwenyezi Mungu pekee anapanga vipi na lini unakuja duniani na unaondokaje duniani,” amesema Rais Samia

Amesema, mara ya mwisho, “nimeonana na Mhandisi Patrick Mfugale, kwenye daraja la JPM pale Busisi, Mwanza. Nilimkuta mzima na makini. Lakini alilolipanga mwenyezi Mungu sisi hatuwezi kulipinga.”

Rais Samia amesema “ukibahatika kupata umri, lazima tuache alama kokote na katika nafasi yoyote tutakayokuwa. Kila mmoja anapaswa kutumia kipawa chake kuacha alama na kila mmoja akifanya hivyo, nchi yetu itapiga hatua.”

Kiongo huyo mkuu wa nchi, ametoa pole kwa familia, wafanyakazi wenzake, ndugu jamaa na marafiki kwa kuondokewa na Mhandisi Mfugale.

Awali, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk. Leonard Chamliho amesema, asubuhi ya tarehe 29 Juni 2021, Mhandisi Mfugale aliamka salama kama siku zingine za kazi na kwenda kazini.

Amesema, kulikuwa na kikao kilichokuwa kikiongozwa na katibu mkuu “na mimi nilikwenda Bungeni” kuhudhulia vikao vya Bunge.

“Wakati kikoa kikiendelea, Mhandisi Mfugale alimweleza katibu mkuu kuwa anajisikia vibaya, akaomba kwenda kupumzika na kwenda kupumzika ofisi ya katibu mkuu wa ujenzi.”

“Alipofika alikaa katika kiti na aliomba kiyoyozi kiongezwe. Lakini hali yake ilibadilika,” amesema

Amesema, kutokana na hali hiyo, gari liliandaliwa kumpeleka Hospitali ya Benjamin Mkapa “na katibu mkuu akawasiliana na katibu mkuu wizara ya afya ili kuandaa madaktari, walipofika pale walikuta madakatari wamejianfaa na baada ya kufanya uchunguzi mfupi, walibaini tayari amekwisha kufariki.”

error: Content is protected !!