RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewaeleza wajumbe wa mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA), kwamba Serikali yake imefanikiwa kudumisha amani na utulivu wa kisiasa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Rais Samia ameyasema hayo leo Alhamisi, tarehe 23 Septemba 2021, akihutubia mkutano huo uliofanyika nchini Marekani na kurushwa mubashara na vituo mbalimbali vya runinga ikichukua takribani dakika sizizozidi 20.
Kiongozi huyo wa Tanzania ameyasema hayo, wakati akielezea jitihada zilizochukuliwa na Serikali yake, katika kuinua ukuaji uchumi ulioshuka kutokana na janga la Ugonjwa wa Korona (UVIKO-19).
Mbele ya wajumbe wa mkutano huo wakiwemo wakuu wa nchi zaidi ya 100 duniani, Rais Samia amesema, Serikali yake imefanya kazi kubwa kuimarisha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji, sambamba na kuimarisha utawala wa sheria, haki za binadamu na demokrasia.
“Wakati tunaendelea taratibu kurekebisha shughuli za kiuchumi zilizoathirika na UVIKO-19, Serikali inaendelea kufanya kazi kubwa ya kuimarisha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji zaidi.”
“Tunafahamu uhusiano uliopo kati ya ukuaji uchumi na utawala bora, tumefanikiwa kudumisha amani na utulivu wa kisiasa, kuimarisha demokrasia pamoja na kujali utawala wa sheria na haki za binadamu,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema, janga la korona limeathiri ukuaji wa uchumi wa Tanzania na kabla halijatokea, ukuaji wake ulikuwa unakadiriwa kuwa asilimia 6.9, lakini kwa sasa inakadiriwa kukua kwa asilimia 5.4.
Amesema sekta ya utalii imeathirika kwa kiasi kikubwa na janga hilo, kufuatia hatua ya nchi mbalimbali kusitisha safari za kimataifa, ili kuzuia kusambaa kwake.
Rais Samia ameziomba jumuiya za kimataifa kuzisaidia nchi zinazoendelea chanjo ya UVIKO-19, kwani hatua hiyo sio tu itasaidia kupunguza kasi ya maambukizi yake, bali itaokoa maisha ya watu.
Leave a comment