October 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia: Serikali itagharamikia matibabu ya Profesa Jay

Spread the love

 

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema, kuanzia sasa Serikali itagharamia matibabu yote anayopata aliyekuwa Mbunge wa Mikumi (Chadema), Joseph Haule maarufu Profesa Jay anayetibiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam. Anaripoti Danson Kaijage…(endelea).

Hayo yamesemwa leo Ijumaa, tarehe 11 Februari 2022 na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alipofika kumjulia hali msanii huyo wa Hip Hop na kuwasilisha salamu za Rais Samia.

“Nimefika kuleta salamu za Rais Samia Suluhu Hassan ambaye yupo safarini nje ya nchi, amesema anatambua mchango wa Profesa Jay akiwa mbunge wa Mikumi lakini pia kazi zake za sanaa ambazo zimehamasisha vijana wengi kujiajiri kupitia muziki,” amesema Ummy

Amesema, “hivyo kuanzia sasa Serikali itagharamia matibabu yake hadi hapo ataporuhusiwa kutoka hospitalini na ninauagiza uongozi wa hospitali kuleta bili zote wizarani kuanzia sasa.”

Aidha, amesema Rais anatoa pole za kuuguza kwa familia ya Profesa Jay na anamtakia kila la heri katika matibabu anayoendelea nayo, apone haraka ili aendelee na shughuli zake.

Kwa upande wake, Grace Mgonjo, mke wa Profesa Jay, amemshukuru Rais Samia na kusema amefanya jambo kubwa sana kwa familia yake na kuongeza hawajajuta kufuata matibabu Hospitali ya Taifa Muhimbili.

“Naushukuru sana uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kuwa tangu tulipofika hapa, walitupokea vizuri sana na hatujawahi kujutia kuwa hapa” amesema Grace.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru amemuhakikishia Waziri Ummy kuwa amepokea maelekezo na atayatekeleza vizuri.

Katika hatua nyingine Waziri Ummy amewapongeza madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kazi kubwa wanayoifanya katika utoaji wa matibabu ya kibingwa yanayotolewa kwa Watanzania na kuahidi kutatua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo katika kufanya kazi.

error: Content is protected !!