Spread the love

 

RAIS Samia Suluhu Hassan, amewaomba viongozi wa dini waendelee kuiombea Serikali ili aendelee kuongoza kwa uadilifu, haki pamoja na kukidhi matamanio ya Watanzania. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mbeya … (endelea).

Mkuu huyo wa nchi, ametoa wito huo leo Jumanne, akizungumza na viongozi wa dini walioshiriki kongamano la kumuombea lililofanyika jijini Mbeya, kwa njia ya simu.

“Kwa hiyo mimi niwashukuru viongozi wa dini na kamati zote za amani, niwatie moyo muendelee kunifanyia hivyo. Mliombee Taifa, mtuombee na viongozi tuweze kuongoza kwa uadilifu, tuongoze kwa haki, tuongoze kama matamanio ya Watanzania. Nategemea ushirikiano wenu,” amesema Rais Samia na kuongeza:

“Nawashukuru sana kwa kongamano mnalofanya, nashukuru sana kwa kweli Taifa linawategemea sana viongozi wa dini kwa maombi, sala na dua zenu. Ndiyo maana tunaweza kufanya tunayofanya.”

Akijibu salamu hizo, Mwenyekiti wa Kongamano la Viongozi wa Dini la Kumuombea Rais Samia, Askofu Donald Mwanjoka, amesema wamechukua hatua hiyo baada ya kuguswa na uongozi wake.

“Nasi tunafanya hivyo tumeguswa na uongozi wako unavyoongoza tangu umeingia madarakani. Tumekusanyika hapa tuendelee kuubeba mpaka tunafika mahali tunasema kwamba ingekuwa kuna rais wa dunia, tungekuchagua uwe rais wa dunia,” amesema Askofu Mwanjoka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *