May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia: Nguvu kazi ya wanawake haijatumika ipasavyo

Rais Samia Suluhu Hassan

Spread the love

 

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema licha ya kwamba nusu ya watu duniani ni wanawake, bado sehemu kubwa ya dunia haijatoa nafasi stahiki kuitumia ipasavyo nguvu kazi wanawake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Pia amesema wanawake ambao wanafikia asilimia 50 ya nguvu kazi ya Taifa bado ni waathirika wakuu wa mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa yanayotokea katika maeneo mbalimbali.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo tarehe 16 Disemba, 2021 wakati akizindua kamati ya ushauri kitaifa ya utekelezaji wa ahadi za nchi kwenye jukwaa la kizazi chenye usawa.

Akifafanua nguvu kazi hiyo amesema iwapo nguvu kazi ya wanawake itatumika kikamilifu ina uwezo mkubwa wa kuchangia uchumi wa dunia.

“Na wataalam wamepiga hesabu wakakisia kwamba wanawake kama watatumika vizuri duniani wanaweza kuchangia hadi Dola za Marekani trilioni 28 kwa mwaka,” amesema.

Aidha, amesema kamati hiyo ni matokeo ya uteuzi wa Tanzania mwaka 2016 kuwa mmoja wa wajumbe wa jopo la kumshauri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Kin Moon kuhusu uwezeshaji wa mwanamke kiuchumi.

“Wakati ule nikisimamia nchi za ukanda wa Kusini na Mashariki mwa Afrika, tulifanya kazi nzuri,” amesema.

Amsema Tanzania ilishiriki mkutano wa kimataifa wenye lengo la kuleta msukumo mpya katika kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake uliofanyika tarehe 30 Juni hadi 2 Julai mwaka huu kule Paris – Ufaransa ambapo Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango aliniwakilisha.

Amesema Dk. Mpango aliitangazia dunia kwamba Tanzania itatekeleza ahadi kwenye eneo la pili la haki za usawa wa kiuchumi kwa wanawake. Maeneo hayo yapo sita ila Tanzania tumechagua eneo la pili.

“Nilikubali kuwa kinara katika utekelezaji wa eneo la pili kati ya maeneo sita ya Jukwaa la kizazi chenye usawa linalohusu haki za kiuchumi kwa wanawake kwa sababu nafasi hii imetokana na kazi nzuri tuliyoifanya mwaka 2016.

“Tanzania tuliteuliwa kuwa mmoja wa wajumbe wa jopo la kumshauri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Kin Moon kuhusu uwezeshaji wa mwanamke kiuchumi na wakati ule nikisimamia nchi za ukanda wa Kusini na Mashariki mwa Afrika, tulifanya kazi nzuri.

“Kazi ile ndio imezaa jukwaa hili sasa lenye maeneo sita, mojawapo ikiwa ni hili tulilochagua kulisimamia. Ni wazi jukwaa hili ni mwendelezo wa jitihada mbalimbali zinazofanywa na UN katika kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma kimaendeleo,” amesema.

Amesema wameunda kamati hiyo ili kutekeleza lengo namba tano la Malengo ya Maendeleo Endelevu ambalo limefungamana na mambo mengi.

“Kwa hiyo muundo wa kamati yetu tunayoizindua leo ina wajumbe kutoka sekta mbalimbali, ili wote waweze kuchangia na tuone tunakwenda kukamilishaje ahadi zetu zile.

“Ili tuweze kumuinua mwanamke wa Tanzania kiuchumi mambo mengi hapo katikati yahitaji kutekelezeka, kwa hiyo wajumbe wale waliotoka sekta mbalimbali watachangia tuelekee huku,” amesema Rais Samia.

error: Content is protected !!