October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia: Mwanamke sio mtu wa daraja la pili

Spread the love

 

RAIS Samia Suluhu Hassan ameliomba Kanisa la Anglikana Tanzania kuunga mkono dhamira ya Serikali katika kuwainua wanawake kijamii, kiuchumi, kisiasa na kupambana na ukatili, dharau, kejeli na manyanyaso wanayokabiliana nayo. Anaripoti Helena Mkonyi – TUDARCo.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo tarehe 28 Septemba 2021 jijini Dodoma wakati akihutubia katika maadhimisho ya miaka 50 ya Kanisa la Anglikana Tanzania.

Amesema si kwamba serikali imedhamiria kutetea wanawake kwa sababu yeye ni mwanamke bali kwa sababu mwanamke ni kiumbe mwenye haki sawa na mwingine anayezaliwa na binadamu.

“Tunapozaliwa wote tunatoka sawa, kwani kuna mwanaume anasema ametoka na shape ya kichwa yenye akili zaidi, wote tunazaliwa sawa. Kinachotutofautisha ni makuzi na imani katika makabila yetu. Katika mambo mengine, mwanamke ana haki sawa na mwanaume kwenye jamii.

“Tunakubali kuna haki za ki-Mungu, mimi nabeba mimba najifungua… wewe huwezi, kwa hilo nina fahari kwamba Mungu amenipa heshima ya kuleta viumbe duniani, unachofanya wewe ni kunichangia mbegu yako, lakini mengine yote ninafanya mwenyewe, kwa makabila mengine mtoto ni wa mama sio wa baba.

“Kwa hiyo mzigo huo alionipa Mungu ni mkubwa na ni heshima kubwa lazima niheshimiwe kwa sababu nimewaleta mimi, nimewakuza mimi, ukiumwa ni mimi, shibe na raha yako ni mimi.

“Sasa unaponiona kama ni mtu wa daraja la pili, sikuelewi nami nitasimama na hilo, kuwanyanyua wenzangu tuende pamoja, lakini sisi wanawake ni zaidi ya asilimia 50 kwenye nchi hii, mkituacha nyuma, nchi itaendelea lini? Alihoji Rais Samia.

Alisema katika malengo ya kimataifa hakuna mtu ambaye anatakiwa aachwe nyuma kimaendeleo.

“Sasa mnapodogosha wanawake mkawanyima haki zao, mkawaonea kwenye mirathi, mkawanyang’anya ardhi zao maendeleo yanakuja lini?

“Nguvu za kanisa isiwe tu kwenye kuwakopesha wanawake na kulea ma-yatima, lakini pia kujenga heshima ya mwanamke wa Tanzania. Kanisa liseme kwa sauti kubwa. Baba Askofu nomba mniunge nguvu kwenye hilo,” amesema Rais Samia.

Aidha, Askofu Mkuu wa Anglikana Tanzania, Maimbo Mndolwa amesema kanisa hilo linaendelea kuwainga mkono wanawake kwa kuwawezesha kupata mikopo mbalimbali ili kujikwamua kiuchumi

error: Content is protected !!