January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia kuunguruma katika mkutano wa vyama vya siasa

Rais Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa CCM

Spread the love

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano wa wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini Tanzania, unaotarajiwa kufanyika tarehe 16 hadi 17, Desemba 2021, jijini Dodoma. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumamosi, tarehe 4 Desemba 2021 na Mwenyekitu wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania, Juma Ali Khatib.

“Itakumbukwa kuwa, mkutano huo ulikuwa ufanyike tarehe 21, 22 na 23 Oktoba 2021, lakini ukaahirishwa kutokana na sababu za msingi. Hivyo, tumeona ni vyema kuwafahamisha wadau wote kuwa, mkutano huu bado upo na sasa umepangwa kufanyika tarehe 16 na 17, Desemba 2021 katika Jiji la Dodoma kama ilivyokuwa imapangwa awali,” imesema taarifa ya Khatib.

Taarifa hiyo imesema “kutokana na umuhimu wa mkutano huu, tumemualika Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Samia Suluhu Hassan, kuwa mgeni rasmi na kuufungua.”

Taarifa ya Khatib imesema, mkutano huo utatanguliwa na semina ya siku moja kwa wajumbe wa baraza hilo, ambayo itahusu historia na majukumu yake, itakayofanyika tarehe 15 Desemba 2021, jijini humo.

“Mkutano huu ni muhimu, kwani utawezesha wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa kukutana na kubadilishana mawazo na uzoefu, ili kuwezesha Sheria zinazoratibu shughuli za vyama vya siasa hapa nchini kwetu kuboreshwa kama itahitajika, pia kujadili utekelezaji wa sheria hizo sambamba na kudumisha amani,  utulivu, uzalendo, maadili na umoja wa Taifa letu,” imesema taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Khatib, mkutano huo utajumuisha wadau mbalimbali wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa, ikiwemo wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa, viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa ambao siyo wajumbe wa baraza hilo, viongozi wa dini ngazi ya Taifa, Taasisi zisizo za Kiserikali (AZAKI) na wa Serikali,

“Mada tatu zitawasilishwa na wataalamu wabobezi, kisha kujadiliwa na washiriki wa mkutano. Mada zitahusu masuala ya kisheria, demokrasia, siasa, uchumi na maadili ya kitaifa, yanayohusiana na demokrasia ya vyama vingi vya siasa.

Hivyo, Baraza la Vyama vya Siasa linatumia fursa hii, kushauri vyama vya siasa vyote vyenye usajili kamili, kuhudhuria mkutano huo, kwani ni fursa adhimu ya kubadilishana mawazo kuhusu mambo yanayotuhusu. Siasa ni ushawishi na ushawishi hufanikiwa kapitia njia ya mijadiliano,” imesema taarifa hiyo.

error: Content is protected !!