RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali yake imedhamiria kuukwamua mchakato wa marekebisho ya katiba na kwamba muda si mrefu kamati ya ushauri juu ya namna ya kuuendesha itaundwa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Mkuu huyo wa nchi ametoa ahadi hiyo leo Jumanne, tarehe 3 Januari 2023, akizungumza na viongozi wa vyama vya siasa nchini Tanzania, Ikulu jijini Dar es Salaam.
“Nataka kuwaambia Serikali inadhamiria kukwamua mchakato wa marekebisho ya katiba kwa jinsi tutakavyokuja kukubaliana hapo mbele, lakini tuko tayari kuukwamua ili tuanze sasa kamati kadhaa zifanye kazi kuangalia mambo kadhaa,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema mchakato huo utakwenda kulingana na hali halisi ya sasa, kwa kuja na mambo mapya pamoja na kuchukua mazuri yaliyokuwepo kwenye Rasimu ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba na katiba pendekezwa.
“Wengine wanasema tuanze na katiba ya Jaji Warioba, wengine katiba pendekezwa lakini ile ilikuwa 2014 ni miaka nane imepita mambo kadhaa yamebadilika. Lakini kuna mambo yamebadilika wakati ule yalikuwa yanatuongoza, kuna haja ya kuangalia hali halisi ya sasa ikoje,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema kamati ya ushauri juu ya namna ya kufufua marekebisho ya katiba mpya, itakuwa na wajumbe kutoka kwenye makundi mbalimbali, ikiwemo vyama vya siasa, mashirika yasiyo ya kiserikali, na watanzania wanaofanya kazi katika taasisi za kimataifa.
Aidha, amesema mchakato wa marekebisho ya katiba utafanyika kwa ustaarabu ili kuruhusu shughuli nyingine za maendeleo kuendelea.
“Nataka niwaambie hakutakuwa na kamati itakayokuwa, vuguvu leo wapi twendeni wapi leo.Tutakuwa na kamati itakayofanya kazi zake kwa maelekezo tutakayowapa kwamba hadidu rejea ni hizi 12 nendeni yafanyieni kazi. Pahali wapi tutawapangia vizuri tu, lakini sio lile vuguvugu,” amesema Rais Samia na kuongeza:
“Tunataka wakati mchakato unaendelea nchi iko tulivu inaendesha shughuli zake za maendeleo na sio vuguvu ambalo litakwenda kusimamisha kila kitu tunaangalia wote kwenye katiba. Watanzania hawatakuja kushiba kwenye katiba, ikiingia njaa wakulima watakuja kunipigia kelele.”
Leave a comment