October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Samia kuendelea kuboresha maisha ya Watanzania

Spread the love

 

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwa ajili ya uendelezaji na ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya maji, elimu na barabara. Anaripoti Mwanaharusi Abdallah, TUDARCo … (endelea).

Hayo ameyasema jana Ijumaa, tarehe 17 Septemba 2021, akiwa siku ya pili ya ziara yake mkoani Kigoma.

Alikuwa anazungumza na wananchi wa Wilaya za Kasulu na Kibondo baada ya kuzindua ghala la kuhifadhia mazao katika kijiji cha Mvugwe na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa maji Kifura.

Wakati wa uzinduzi huo, Majaliwa alisema Rais Samia ametoa fedha nyingi kwa ajili ya uendelezaji na ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa na lengo la kuboresha maisha ya Watanzania.

Amewataka wananchi wafanye kazi kwa bidii kila mmoja kwenye eneo lake na waendelee kuwa na amani na serikali yao.

Majaliwa alisema ”Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amedhamiria kupeleka huduma mbalimbali za jamii kwa wananchi wote nchini. Huduma hizo ni pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama kwa sababu anajua namna akinamama na vijana wanavyohangaika kutafuta maji.”

Hata hivyo, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoa wa Kigoma, Mathius Mwenda alisema mradi huo wenye thamani ya Sh.2.4 bilioni, mkataba wake ulisainiwa Agosti 2021 na unatarajiwa kukamilika Februari 2022.

Mradi huo utakapokamilika utakuwa na vituo 50 vya kuchotea maji.

Meneja huyo alisema kukamilika kwa mradi huo kunakwenda kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa kijiji cha Kifura hivyo watahakikisha unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyostahiki.

Pamoja na hayo, Majaliwa aliwapongeza wananchi kwa kubuni mradi huo na alisisitiza kuwa wananchi hao waendeleze ushirika wao na watumie ghala hilo kwa ajili ya kuuza mazao.

Pia mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu, Joseph Rwiza alisema mradi huo uliogharimu Sh. 464 milioni unalenga kupunguza upotevu wa mazao, kutunza na kuongeza ubora wa mazao pamoja na kuwepo kwa soko la uhakika na bei yenye tija kwa wakulima.

error: Content is protected !!