RAIS wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan,amesema kuimarika kwa demorasia, utawala wa sheria na haki za binadamu, kumewavutia wawekezaji kutoka Ujerumani kuja kuwekeza nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Mkuu huyo wa nchi ametoa kauli hiyo leo tarehe 31 Oktoba 2023, Ikulu jijini Dar es Salaam, wakati akitoa mrejesho wa masuala aliyozungumza na Rais wa Shirikisho la Ujerumani, Dk. Frank Walter Steinmeier, aliyeko nchini kwa ajili ya ziara ya kikazi itakayofika tamati kesho Jumatano.
“Kuhusu masuala ya demokrasia, haki za binadamu, utawala bora na utawala wa sheria, tumezungumza na Rais Steinmeier na ametupongeza kwamba Tanzania tunaonekana tumetulia kwenye utawala wa sheria na utawala bora ndiyo maana wanavutika wafanyabiashara wa Ujerumani kuja Tanzania kuangalia fursa za uwekezaji,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema katika mazungumzo hayo wamekubaliana kushirikiana katika masuala ya biashara na uwekezaji ili kuimarisha maendeleo ya uchumi na kijamii kwa wananchi wa pande zote.
Amesema, kutokana na mahusiano mazuri katika Tanzania na Ujerumani, wafanyabiashara wa taifa hilo wamewekeza miradi zaidi ya 170 nchini.
Rais Samia ametaja maeneo mengine ambayo Tanzania na Ujerumani zitaendelea kushirkiana, ikiwemo masuala ya usawa wa kijinsia, uwezeshaji wanawake kiuchumi kupitia miradi mbalimbali itakayotekelezwa kwa ushrikiano wa nchi hizo mbili.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema Serikali ya Ujerumani, imekubali kuwasaidia vijana wabunifu katika masuala ya uchumi wa kidigitali.
Leave a comment